• HABARI MPYA

  Tuesday, July 22, 2014

  LOGARUSIC ASAINI MKATABA MPYA SIMBA SC NA KUSEMA; “TIMU ITAKUWA TISHIO MSIMU UJAO”

  Na Samira Said, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mkuu wa Simba SC, Mcroatia Zdravko Logarusic amesaini Mkataba mpya wa mwaka mmoja na kusema kwamba timu hiyo itakuwa bora msimu ujao, ubingwa wa Ligi Kuu ikiwa lengo la kwanza.
  Akizungumza makao makuu ya klabu, Mtaa wa Msimbazi baada ya kusaini Mkataba huo, kocha huyo wa zamani wa Gor Mahia ya Kenya amesema kwamba amefurahi kusaini kandarasi mpya na sasa anaelekeza nguvu zake kwenye kazi. Loga amesema Simba SC itakuwa timu bora msimu ujao na lengo lake kuu ni kuhakikisha inatwaa ubingwa.
  Kocha wa Simba SC, Zdravko Logarusic kulia akisaini Mkataba pembeni ya Makamu wa Rais wa klabu hiyo, Geoffrey Nyange 'Kaburu' leo Msimbazi
  Logarusic kulia akipeana mikono na viongozi wa Simba SC baada ya kupewa Mkataba wake

  Kwa upande wake, Makamu wa Rais Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ aliyesaini Mkataba na kocha huyo amesema kwamba sasa msalaba mkubwa wa Loga ni kuhakikisa Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu msimu ujao linatua Msimbazi.
  Kaburu pia amesema Kocha Msadizi, Suleiman Matola ‘Bin Laden’ naye alisaini Mkataba wa miaka miwili tangu Novemba mwaka jana.
  Loga alijiunga na Simba SC Desemba mwaka jana kwa Mkataba wa miezi sita, lakini uongozi wa klabu hiyo umeridhishwa na kazi yake na kumuongeza mwaka mmoja mwingine.
  Katika hatua nyingine, kiungo wa kimataifa wa Kenya, Paul Mungai Kiongera aliyekuwa awasili nchini leo kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kujiunga na Simba SC, sasa atakuja kesho.
  Mchezaji huyo wa KCB ya Ligi Kuu ya nchini, ameshindwa kuja leo baada ya kukosa ndege, lakini Kamati ya Usajili ya Simba leo ilikuwa inahangaikia nafasi itakayomuwezesha kutua kesho Dar es Salaam.
  Tayari Simba SC imefikia makubalinao na kiungo mwingine Mrundi, Pierre Kwizera ambaye amerejea Ivory Coast kumalizana na klabu yake, Afad Abidjan ili aje kusaini Mkataba.
  Simba SC pia ipo kwenye mazungumzo na klabu za JKT Ruvu, Ruvu Shooting na Coastal Union kwa ajili ya kuwanunua wachezaji Edward Charles, Elias Maguri na Abdul Banda.
  BIN ZUBEIRY inafahamu mazungumzo hayo yanaendelea vizuri na kuna uwezekano wachezaji hao wakahamia Msimbazi kwa ajili ya msimu ujao.
  Kwa upande mwingine, Simba SC itakutana na wachezaji wake ambao bado wana mikataba, lakini haiwahitaji kwa sasa ili kujadiliana nao kuvunja kandarasi hizo.
  Hao ni kipa Abuu Hashimu, beki Hassan Khatib, viungo Abulhalim Humud ‘Gaucho’, Ramadhani Chombo ‘Redondo na washambuliaji Betram Mombeki na Christopher Edward.  
  Tayari Simba SC imefikia makubaliano ya kuachana na beki Mrundi, Kaze Gilbert anayetakiwa na klabu yake ya zamani, Vital’O. Simba SC inatarajiwa kwenda kuweka kambi Zanzibar wiki hii kujiandaa na msimu mpya.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: LOGARUSIC ASAINI MKATABA MPYA SIMBA SC NA KUSEMA; “TIMU ITAKUWA TISHIO MSIMU UJAO” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top