• HABARI MPYA

    Sunday, July 21, 2013

    TEGETE AINUSURU YANGA KUZAMA KWA URA, ZATOKA 2-2 TAIFA AKIPIGA BAO DAKIKA YA 90

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JULAI 21, 2013 SAA 12:23 JIONI
    ANGALAU Yanga wanaweza kujisifu tayari wana timu kuliko wapinzai wao, Simba SC. Baada ya jana URA ya Uganda kuifunga Simba SC mabao 2-1, leo imekwaa kisiki kufuatia kulazimishwa sare ya 2-2 na mabingwa wa Bara, Yanga SC, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Shujaa wa leo; Kipa wa URA, Yassin Mugabi akiwa amejibweteka chini huku Jerry Tegete akikimbia kushangilia bao la kusawazisha aliloifungia Yanga jioni hii Uwanja wa Taifa 

    Lakini haikuwa sare nyepesi, kwani mabingwa wa Tanzania Bara walilazimika kuhaha kusaka mabao ya kusawazisha hadi walipojitoa uwanjani salama dakika ya 90 kwa bao la Jerry Tegete.
    Mkombozi; Mshambuliaji wa Yanga, Jerry Tegete akikabiliana na mabeki wa URA. Tegete leo ameinusuru Yanga kuzama mbele ya URA kwa kufunga bao la kusawazisha dakika za lala salama.

    Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa Kennedy Mapunda aliyesaidiwa na Iddi Maganga na Othman Othman, hadi mapumziko URA tayari walikuwa mbele mkwa bao 1-0.
    Bao hilo lilifungwa dakika ya 42 na Litumba Yayo, ambaye jana Watoza Kodi hao wa Uganda wakiilaza Simba SC 2-1, alifunga mabao yote. 
    Kipindi cha kwanza URA ndio waliotawala mchezo kwa kucheza kwa kasi nzuri, uelewano mzuri na kushambulia kwa nguvu, wakati Yanga SC walionekana kukosa mipango.
    Kipindi cha pili, URA walianza tena vyema na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 61, mfungaji Yayo tena akiweka rekodi ya kufunga mabao manne Taifa ndani ya siku mbili.
    Kocha Mholanzi, Ernie Brandts alilazimika kufanya mabadiliko baada ya bao hilo, akiwaingiza Haruna Niyonzima kuchukua nafasi ya Said Bahanuzi wingi ya kulia, Bakari Masoud kuchukua nafasi ya Hamisi Thabit na Abdallah Mnguli ‘Messi’ kuchukua nafasi ya Shaaban Kondo. 
    Mabadiliko hayo yaliisaidia Yanga SC ambayo iliongeza kasi ya mashambulizi na kufanikiwa kuchomoa mabao yote, moja baada ya lingine.
    Mrundi Didier Kavumbangu alianza dakika ya 66 akiunganisha krosi ya beki Juma Abdul kabla ya Tegete kusawazisha dakika ya 90 baada ya kuwazidi nguvu na maarifa kipa wa URA, Yassin Mugabi na mabeki wawili.
    Alivyofunga; Tegete akikabiliana na mabeki wa URA na kipa wao kabla ya kufunga
    Tegete ambaye ana muda mrefu hajaifungia bao Yanga, alipagawa mno kwa kufunga bao muhimu leo na kwenda kushangilia mbele ya mashabiki kwa ishara mbili- kuomba msamaha na pili kuwaambia anaipenda Yanga kwa kuibusu nembo ya klabu iliyopo kwenye jezi sambamba na kuwapa ishara ya kuwataka watulie, mpira hauhitaji papara. 
    Kikosi cha Yanga SC leo kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Ibrahim Job, Rajab Zahir 14, Salim Telela 2, Said Bahanuzi/Niyo, Hamisi Thabit 28/Bakari Masoud, Jerry Tegete, Didier Kavumbangu na Shaaban Kondo18/Abdallah Mguli.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: TEGETE AINUSURU YANGA KUZAMA KWA URA, ZATOKA 2-2 TAIFA AKIPIGA BAO DAKIKA YA 90 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top