• HABARI MPYA

  Jumamosi, Julai 27, 2013

  KAPOMBE AITUMIA SALAMU NZITO STARS KAMPALA, KIKOSI KINACHOANZA HIKI HAPA NA TIMU TAYARI IPO NAMBOOLE

  Na Mahmoud Zubeiry, Kampala, IMEWEKWA JULAI 27, 2013 SAA 8:20 MCHANA
  SAA chache kabla haijashuka dimbani, Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa, kumenyana na wenyeji Uganda, timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imetumiwa salamu za heri na beki wake, Shomary Kapombe aliye Uholanzi kwenye majaribio.
  Kapombe ametuma salamu hizo kupitia ukurasa wake wa Faceboo, akisema; “Go Taifa Stars, go Bocco, go Ngassa, go Chanongo, go Msuva, go Kiemba...,”.
  Go Stars;Kapombe ameitumia salamu 
  za heri Stars kutoka Uholanzi alipo

  Ujumbe huu pamoja na kuitakia heri Stars katika mchezo wa jioni hii kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, pia unawahamasisha baadhi ya wachezaji aliowataja.
  Kapombe anawataka John Bocco ‘Adebayor’, Mrisho Ngassa, Haroun Chanongo, Simon Msuva na Amri Kiemba na wenzao wajitume kubeba jahazi la Stars ifuzu CHAN mwakani Afrika Kusini.
  Kapombe alikuwepo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki mbili zilizopita wakati Stars inafungwa 1-0 na Uganda katika mchezo wa kwanza na baada ya hapo, akaenda Uholanzi kwenye majaribio.
  Mchezaji mwingine anayekosekana leo, aliyecheza mechi ya kwanza ni Mwinyi Kazimoto aliyetorokea Qatar.
  Kikosi cha Stars kinachotarajiwa kuanza jioni hii ni; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, David Luhende, Aggrey Morris, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco ‘Adebayor’, Amri Kiemba na Mrisho Ngassa.
  Wawili tu; Kikosi cha Stars kilichocheza mechi ya kwanza na Uganda Dar es Salaam. Kutoka kulia waliosimama Kaseja, Yondan, Bocco, Nyoni, Kiemba na Morris. Waliochuchumaa kutoka kulia Kapombe, Ngassa, Kazimoto, Domayo na Sure Boy. Kapombe na Kazimoto hawapo na badala yao watacheza Luhende na Chuji.

  Katika benchi watakuwepo Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Luizio, Mudathir Yahya, Nadir Cannavaro, Haroun Chanongo, Simon Msuva na Vincent Barnabas.
  Tayari Stars imekwishaingia Uwanja wa Mandela, kiasi cha saa moja iliyopita na muda si mrefu itaingia uwanjani kuamsha misuli. Mungu ibariki Stars, ibariki Tanzania. Amin.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: KAPOMBE AITUMIA SALAMU NZITO STARS KAMPALA, KIKOSI KINACHOANZA HIKI HAPA NA TIMU TAYARI IPO NAMBOOLE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top