• HABARI MPYA

  Jumapili, Julai 28, 2013

  KASEJA ASEMA MAKINDA WAMEIUA STARS, AWATAKA MASHABIKI WABADILIKE JUU YA MTAZAMO WA WAKONGWE

  Na Mahmoud Zubeiry, Kampala, IMEWEKWA JULAI 28, 2013 SAA 2:26 ASUBUHI
  NAHODHA wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Juma Kaseja amewataka mashabiki wa soka nchini kubadilisha mitazamo yao kwamba wachezaji chupikizi ndiyo wanaofaa kuliko wakongwe.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana mjini hapa, Kaseja alisema kwamba mashabiki wamekuwa wakitaka sana wachezaji chipukizi wapewe nafasi, lakini ukweli ni kwamba hawamudu kazi.
  Alipotezwa;; Juma Kaseja akipishana na mkwaju wa penalti wa Brian Majwega jana, baada ya David Luhende kuunawa mpira

  “Tusaidieni kuwaelimisha mashabiki, wao wanataka sana wachezaji chipukizi, lakini nadhani mmeona leo, hawawezi. Wanahitaji kupewa muda wakomae taratibu. Hata sisi tulipokuwa chipukizi, tulikomazwa taratibu,”alisema Kaseja.
  Ingawa Kaseja hakuweka wazi, lakini inaonekana alikuwa anawazungumzia wachezaji chipukizi walivyoigharimu Stars jana ikitolewa na Uganda katika michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, ikafungwa na Uganda mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa.
  Alifanya kazi; Juma Kaseja akienda hewani kudaka mpira wa juu

  Kwa matokeo hayo, Tanzania inayofundishwa na kocha Mdenmark, Kim Poulsen imetolewa kwa jumla ya mabao 4-1, baada ya wiki mbili zilizopita kufungwa 1-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Beki chipukizi, David Luhende aliyeitwa Stars kwa mara ya kwanza safari hii, aliunawa mpira akiwa peke yake- baada ya kushindwa kuumilii vyema na kusababisha penalti, wakati huo timu hizo zikiwa zimefungana 1-1 na Brian Majwega akaifungia Uganda bao la pili.
  Uchochoro; David Luhende jana watu wanapitiliza tu na akaunawa mpira akiwa peke yake kusababisha penalti iliyoiua Stars

  Kiungo chipukizi, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ aliyepandishwa timu hiyo Mei mwaka jana, alijaribu kuwapiga chenga wachezaji wawili wa Uganda, wakati huo wachezaji karibu wote wa Tanzania wamepanda kufuata shambulizi la kona, akapokonywa mpira na likafanywa shambulizi la kushitukiza, Stars ikafungwa bao la tatu.
  Wachezaji wengine chipukizi walioingizwa kipindi cha pili, Simon Msuva na Haroun Chanongo walishindwa kuisaidia timu kubadilisha matokeo japo kidogo.   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: KASEJA ASEMA MAKINDA WAMEIUA STARS, AWATAKA MASHABIKI WABADILIKE JUU YA MTAZAMO WA WAKONGWE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top