• HABARI MPYA

  Alhamisi, Julai 25, 2013

  MNIGERIA WA YANGA APANDISHWA NDEGE KUREJEA NYUMBANI, SHUGHULI IMEISHA...KIIZA AREJESHWA DAR KWA MJADALA ZAIDI

  Na Prince Akbar, IMEWEKWA JULAI 25, 2013 SAA 3: 32 USIKU
  HAMISI Friday Kiiza tayari tupo Dar es Salaam tangu jana na wakati wowote anaweza kusaini Mkataba wa miaka miwili kuendelea kuichezea Yanga SC, huku mshambuliaji Mnigeria, Ogbu Brendan Chukwudi anapanda ndege kesho kurejea nyumbani. 
  Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga SC, Abdallah Ahmed Bin Kleb ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, Kiiza amerejea Dar es Salaam na watamalizana wakati wowote.
  Bin Kleb pia amesema Mnigeria Chukwudi wameamua kuachana naye kwa sababu wanaona maumivu yake ni ya muda mrefu na kipindi kilichobaki kabla ya dirisha la usajili la Bara kufungwa ni kidogo.
  Amerudishwa; Hamisi Kiiza kushoto akizungumza na Bin Kleb. Diego huyo wa Kampala atasaini Mkataba na Yanga wakati wowote

  “Ni mchezaji mzuri, lakini hatuna namna kwa sababu ana maumivu mengi na tunahitaji watu wa kutufanyia kazi kwa wakati huu,”alisema Kleb.
  Chukwudi aliyewasili wiki iliyopita Dar es Salaam kutoka klabu ya Heartland FC ya Nigeria, ameshindwa kupewa Mkataba Yanga baada ya kukumbana na maumivu mfululizo akiwa mazoezini.
  Aliumia mara mbili mazoezini kabla ya kuumia tena akiwa anapasha misuli moto kujiandaa kuichezea Yanga SC mechi ya kwanza, dhidi ya URA mwishoni mwa wiki. 
  Lakini tayari Yanga imesajili mshambuliaji mwingine mzawa, Hussein Javu aliyesaini Mkataba wa miaka miwili kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro na leo asubuhi ameanza mazoezi kwenye Uwanja wa Sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
  BIN ZUBEIRY inafahamu Javu ameigharimu Yanga SC zaidi ya Sh. Milioni 60 kwa pamoja fedha alizopewa za usajili na ambazo klabu yake, Mtibwa imelipwa.
  Javu ni kati ya washambuliaji wazuri Tanzania kwa sasa, ambaye kwa misimu mitatu amekuwa mwiba dhidi ya vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga zinapokutana na timu hiyo ya Manungu.
  Habari kutoka kwenye mazoezi ya Yanga SC leo, zimesema kwamba kocha Brandts amevutiwa mno na uwezo wa Javu na kwa ujumla amefurahia ujio wake.
  Shughuli imeisha; Chukwudi anarejea nyumbani kesho baada ya mambo kumuendea kombo Yanga SC

  Javu ni mchezaji mwenye uzoefu ambaye amekuwa akiitwa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars tangu enzi za Mbrazil, Marcio Maximo ingawa mbele ya Mdenmark, Kim Poulsen hajawahi kupata nafasi.  
  Kusajiliwa kwa Javu, kunaongeza ushindani katika safu ya ushambuliaji ya Yanga SC, kwani sasa inakuwa na watu watano, wengine ni Jerry Tegete, Didier Kavumbangu, Shaaban Kondo na Kiiza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: MNIGERIA WA YANGA APANDISHWA NDEGE KUREJEA NYUMBANI, SHUGHULI IMEISHA...KIIZA AREJESHWA DAR KWA MJADALA ZAIDI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top