• HABARI MPYA

  Jumapili, Julai 28, 2013

  COASTAL UNION YAUWA MNYAMA MKWAKWANI, YAILAZA SIMBA 1-0 JIONI HII

  Na Oscar Assenga, Tanga, IMEWEKWA JULAI 28, 2013 SAA 12:11 JIONI
  BAO pekee la kiungo wa kimataifa wa Kenya, Crispin Odula, jioni hii limeipa Coastal Union ushindi wa 1-0 dhidi ya Simba SC ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa nyumbani, Mkwakwani, Tanga. 
  Huo unakuwa ushindi wa pili mfululizo kwa Coastal inayofundishwa na Mzanzibari, Hemed Morocco kwenye Uwanja wa nyumbani, baada ya Jumatano kuifunga 1-0 URA ya Uganda, bao pekee la mshambuliaji mpya kutoka Polisi Morogoro, Kenneth Masumbuko.
  Kwa Simba SC, iliyo chini ya mwalimu mkongwe, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ hicho ni kipigo cha pili mfululizo, baada ya wiki iliyopita kufungwa 2-1 na URA Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Katika mchezo wa leo uliovuta mashabiki wengi uwanjani, Coastal ilipata bao lake hilo pekee dakika ya 53 baada ya kuipasua vizuri ngome ya Simba SC, iliyoongozwa na beki kutoka Afrika Kusini, Vincent Mabusela.
  Simba SC ilipata nafasi mbili ambazo ilishindwa kuzitumia, moja Sino Augustino alipiga shuti kali likagonga mwamba baada ya Wekundu wa Msimbazi kufanya shambulizi la kushitukiza- na Abdulhalim Humud ‘Gaucho’ dakika ya 16 naye aliipasua ngome ya Coastal, lakini akapiga shuti kali juu ya lango.
  Zahor Pazi aliisumbua mno ngome ya Coastal alipoingia kuchukua nafasi ya Sino kipindi cha pili, lakini hakuweza kufunga tu.
  Kikosi cha Coastal Union leo kilikuwa; Shaaban Kado, Mbwana Bakari/Hamad Hamisi dk84, Othman Omary, Juma Nyosso, Marcus Ndahele, Jerry Santo, Uhuru Suleiman/Abdi Banda dk73, Crispin Odula/Suleiman Kassim ‘Selembe’ dk54, Keneth Masumbuko, Haruna Moshi ‘Boban’ na Danny Lyanga.
  Simba SC; Abbel Dhaira, Nassor Masoud ‘Chollo’, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Rahim Juma, Vincent Mabusela/Miraj Adam dk78, Jonas Mkude, Said Ndemla/Marcel Kaheza dk 25, Abdulhalim Humud, Sino Augustino/Zahor Pazi dk46, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ na Ramadhani Singano ‘Messi’/Twaha Shekuwe.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: COASTAL UNION YAUWA MNYAMA MKWAKWANI, YAILAZA SIMBA 1-0 JIONI HII Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top