• HABARI MPYA

    Saturday, July 20, 2013

    SIMBA SC YAFUNGWA 2-1 NA URA, MSHAMBULIAJI MPYA MSIMBAZI AFUNGA BONGE LA BAO NA KUSHANGILIA KAMA YEKINI

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JULAI 20, 3013 SAA 12: 30 JIONI
    SIMBA SC jioni ya leo imechapwa mabao 2-1 na URA ya Uganda katika mchezo wa kirafiki kujiandaa na msimu mpya, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa Michael Magori aliyesaidiwa na Iddi Likongoti na Omar Mfaume wa Dar es Salaam, hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
    Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji mpya, Betram Mombeki aliyegongeana pasi vizuri na Marcel Boniventura. Mombeki alichukua pasi ya Singano ‘Messi’ akawapangua mabeki wa URA kabla ya kumpelekea pasi fupi Marcel aliyemrudishia mshambuliaji huyo mpya, akaunganisha nyavuni.
    Kama Yekini; Mombeki baaada ya kufunga akishangilia ndani ya nyavu

    Baada ya kufunga bao hilo, Mombeki alikwenda kushangilia kwa staili ya mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Nigeria, marehemu Rashid Yakini kwa kuingia kucheza ndani ya nyavu.  
    Kwa ujumla Simba SC ndio waliotawala mchezo kipindi cha kwanza wakionana vema na kucheza kwa kujiamini, wakati kwa URA iliwawia vigumu kuupenya ukuta wa Wekundu wa Msimbazi, uliokuwa chini ya Mganda mwenzao, Samuel Ssenkoom leo.
    Kipindi cha pili, Simba SC inayofundiahwa na kocha mzalendo, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ ilirudi vizuri na kuendelea kuwapa raha mashabiki wake kwa soka maridadi. 
    Hata hivyo, kibao kiliigeukia Simba SC baada ya mshambuliaji wake, Mombeki kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kiwiko beki wa URA, Jonathan Mugabi dakika ya 51, ambaye alishindwa kuendelea na mchezo.
    Baada ya hapo kwa kuwa tayari mshambuliaji mwingine aliyekuwa akiisumbua ngome ya URA, Zahor Pazi alikuwa amekwishatolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Twaha Ibrahim, mabeki wa timu ya Uganda, wakiongozwa na Joseph Owino na Derick Walullya walianza kupanda zaidi kusaidia mashambulizi.
    URA ilipata bao lake la kusawazisha dakika ya 60 mfungaji Lutimba Yayo akiunganisha krosi nzuri ya Walullya.
    Wakati SImba wakijaribu kusaka bao la pili, Yayo tena akaifungia URA bao la ushindi dakika ya 75.  
    Hakukuwa tena na mashambulizi ya uhai kwa upande wa Simba na URA hawakuweza kumfunga Mganda mwenzao, Abbel Dhaira zaidi ya mara mbili. 
    Simba SC; Abbel Dhaira, Nassor Masoud ‘Chollo’, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Rahim Juma/Sino Augustino, Samuel Ssenkoom, Jonas Mkude, Ramadhani Singano/Miraj Adam, William Lucian, Betram Mombeki, Zahor Pazi/Twaha Ibrahim na Marcel Boniventura.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA SC YAFUNGWA 2-1 NA URA, MSHAMBULIAJI MPYA MSIMBAZI AFUNGA BONGE LA BAO NA KUSHANGILIA KAMA YEKINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top