• HABARI MPYA

  Jumatano, Julai 24, 2013

  UJUMBE WA SIMU WAMVURUGA SURE BOY UGANDA, UTAMUONEA HURUMA

  Na Mahmoud Zubeiry, Kampala, IMEWEKWA JULAI 24, 2013 SAA 4:50 USIKU
  KIUNGO Salum Abubakar ‘Sure Boy’ aliwasili vizuri na mwenye furaha Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Entebe, nchini Uganda lakini ghafla akabadilika baada ya kupokea ujumbe kwenye yake ya mkononi.
  Kiungo huyo wa Azam FC, aliwasili akiwa mwenye furaha na anayecheka na wenzake kwenye Uwanja huo wa ndege kabla ya kutoka nje kupanda basi.
  Mtu wa mwisho kuwasiliana na Sure kabla ya kutoka nje alikuwa Mrisho Ngassa ambaye alionekana kama anayempa ujumbe uliotumwa kwenye simu yake (Ngassa).
  Kulikoni Sure? Kiungo wa Stars, Salum Abubakar kulia ameshika tama kwenye basi, baada ya kusoma ujumbe wa simu

  Mara tu baada ya kupanda basi, Sure alitoa simu yake na kusoma ujumbe na ghafla akabadilika na kuwa mnyonge hadi kushika tama. Aliendelea kuwa hivyo hadi basi hilo linaondoka kuelekea Kampala, ambako Stars imefikia katika hoteli ya Mt. Zion.
  Stars imetua hapa jioni ya leo kwa ajili ya mchezo wa marudiano ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee dhidi ya wenyeji, Uganda, The Cranes Jumamosi Uwanja wa Mandela, Namboole mjini Kampala.
  Sure Boy alikuwa mwenye furaha baada ya kuteremka kwenye ndege, hapa akizungumza na mchezaji mwenza wa Azam FC, Aggrey Morris kulia

  Stars iliyofungwa 1-0 katika mchezo wa kwanza wiki iliyopita mjini Dar es Salaam, sasa inatakiwa kushinda 2-0 ili kukata tiketi ya kwenda Afrika Kusini mwakani, zitakapopigwa Fainali za CHAN, au ishinde 1-0 na mchezo uamuliwe kwa mikwaju ya penalti.
  Imekuja ikitokea mjini Mwanza ilipoweka kambi ya siku 10 baada ya mechi ya kwanza. Ilipokuwa Mwanza, Stars ilikuwa kifanya mazoezi ya kupiga penalti, kujiweka tayari kwa zoezi hilo endapo litatokea. 
  Kikosi cha Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kilichotua hapa ni makipa Juma Kaseja, Mwadini Ali na Ali Mustafa. Mabeki ni Aggrey Morris, David Luhende, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Nadir Haroub na Vincent Barnabas.
  Viungo ni Amri Kiemba, Athuman Idd, Frank Domayo, Haroun Chanongo, Khamis Mcha, Mudhathir Yahya, Salum Abubakar na Simon Msuva. Washambuliaji ni John Boko, Juma Luizio na Mrisho Ngasa.
  Mrisho Ngassa alikuwa mtu wa mwisho kuzungumza na Sure kabla hajapanda basi. Hapa anaonekana kama anayemsomea ujumbe wa simu

  The Cranes nayo imeendelea na mazoezi jioni ya leo Uwanja wa Namboole na kocha wake, Mserbia Milutin Sredojevic ‘Micho’ amesema kwamba kikosi chake kipo tayari kukamilisha kazi kilichoianza Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: UJUMBE WA SIMU WAMVURUGA SURE BOY UGANDA, UTAMUONEA HURUMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top