• HABARI MPYA

  Jumatatu, Julai 22, 2013

  MNIGERIA YANGA SC SASA AMEKALIA KUTI KAVU

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JULAI 22, 2013 SAA 3:35 ASUBUHI
  MSHAMBULIAJI Mnigeria aliye katika majaribio Yanga SC, Brendan Ogbu Chukwudi amesema kwamba hana namna zaidi ya kupumzika na kupata tiba kwa sasa, baada ya kuandamwa na majeruhi.
  Chukwudi aliyetua nchini usiku wa kuamkia Jumanne iliyopita, ilikuwa aanze katika mechi ya jana ya kirafiki dhidi ya URA ya Uganda, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, lakini akaumia wakati wa kupasha misuli moto na kuondolewa katika mchezo huo ulioisha kwa sare ya 2-2.
  “Inasikitisha, nimeumia tena. Safari hii ni kifuniko cha goti. Sijui ni nini hapa, ila hakuna namna nyingine zaidi ya kupumzika na kupata tiba kwa sasa,“alisema Chukwudi jana akiwa anatazama mechi hiyo.
  Kuti kavu: Mshambuliaji Ogbu Brendan Chukwudi anaandamwa na majeruhi akiwa katika majaribio Yanga SC na sasa amekalia kuti kavu Jangwani. Hapa alikuwa anaangalia mechi jana baada ya kuumia.

  Kwa upande wake kocha wa Yanga SC, Mholanzi Ernie Brandts alisema anampa muda Mnigeria huyo apone na kuonyesha uwezo wake mazoezini, ilia atoe baraka zake kwa uongozi asajiliwe.
  Naye Daktari wa Yanga SC, Nassor Matuzya amesema inaonekana mchezaji huyo ana matatizo mengi na ambayo ni ya muda mrefu kwake.
  “Kwanza ilikuwa ni kifundo cha mguu. Tumehangaika naye na akawa anacheza, sasa hivi tena linaibuka la kufuniko cha goti. Kwa kweli hii hali inatusikitisha na hatujui la kufanya kwa sasa,”alisema.
  Lakini Dk Matuzya pia akaushauri uongzi wa Yanga SC kwamba kaunzia sasa uweke utaratibu wa kuwapima afya wachezaji kabla ya kuwaleta kwenye timu, ili kuepuka gharama zisizo za lazima.
  Kinachoonekana ni kama benchi la Ufundi la Yanga SC halijaridhishwa na mchezaji huyo na wanahofia tu kuwaambia ukweli viongozi hadi watakapojionea wenyewe.
  Akijua kabisa mchezaji huyo ni majeruhi na hayuko fiti- lakini kocha Brandts jana alitaka kumpanga Chukwudi kama si kuumia wakati anapasha misuli moto.
  Kulingana na wasifu wake na rekodi zake- Chukwudi aliyetokea Heartland FC ya Nigeria, ni mchezaji mzuri na hadi msimu uliopita alikuwa moto katika Ligi Kuu ya Nigeria kiasi hadi cha kuitwa timu ya taifa ya nchi hiyo, Super Eagles.    
  Mchezaji huyo wa zamani wa Enugu Rangers ya Nigeria sasa mustakabali wake ni tata Yanga SC- haijulikani kama uongozi utacheza kamari kwa kuamua kumsajili na kumtibu au kuachana naye na kutafuta mchezaji mwingine.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: MNIGERIA YANGA SC SASA AMEKALIA KUTI KAVU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top