• HABARI MPYA

  Jumatatu, Julai 22, 2013

  SAMATTA AENDELEA KUNG'ARA AFRIKA, AIPIGIA BAO MUHIMU UGENINI MAZEMBE CAF

  Na Prince Akbar, IMEWEKWA JULAI 22, 2013 SAA 7:20 USIKU
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ‘Sama Mabao’ wikiendi hii ameendelea kung’ara katika michuano ya Afrika, baada ya kuifungia bao ugenini timu yake, TP Mazembe ya DRC ikitoa sare ya 1-1 Entente Setif ya Algeria.
  Wenyeji ndiyo waliosota hadi kukomboa bao kwenye Uwanja wa Mei 8, 1945 katika mchezo wa ufunguzi Kundi B, Kombe la Shirikisho Afrika uliopigwa usiku wa Ijumaa.
  Timu hiyo ya Lubumbashi ilikuwa katika wakati mgumu kwa dakika 15 za mwanzo kutokana na wenyeji, Setif kuanza kwa kasi wakisaka bao la mapema.
  Sama Mabao; Mbwana Samatta ameendelea kung'ara Afrika

  El Aid Madouni alikaribia kuwafungia bao mabingwa hao wa 2010 Kombe la Shirikisho dakika ya saba, lakini mpira alioupiga kwa kichwa ukapaa juu ya lango la kipa wa Mazembe, Muteba Kidiaba pembeni.
  Baada ya hapo, Mazembe nao walizinduka na kushambulia na kukosa mabao kipindi cha kwanza, lakini timu hizo zilikwenda kupumzika zikiwa hazijafungana.
  Kipindi cha pili, Mazembe ilinusurika kufungwa bao la mapema dakika ya kwanza tu, wakati mshambuliaji wa Setif, Kalid Gourmi alipopiga juu shuti lake dhaifu.
  Dakika tano baadaye, kiungo wa Ghana, Gladson Awako alipoteza nafasi nzuri ya kufunga akiwa amebaki na kipa tu wa Setif, Sofiane Khedaira.
  Dakika ya 81 nyota wa Mazembe na mmoja wa wapachika mabao hodari kwenye michuano ya Afrika, Mtanzania Mbwana Samatta aliwafungia wageni bao.
  Hata hivyo, bao hilo la Mazembe halikudumu sana, kwani dakika mbili baadaye, beki Mourad Delhoum alisawazisha.
  Timu hizo mbili sasa zinalingana kwa pointi baada ya mechi zao za kwanza Kundi B bila ya matokeo ya mechi ya jana nchini Morocco kati ya wenyeji, FUS Rabat dhidi ya CA Bizertin ya Tunisia mjini Rabat.
  Wakati huo huo, Mazembe inarejea nyumbani ambako itaikaribisha FUS Agosti 4, wakati Setif itakwenda Tunisia kuwafuata Bizertin wikiendi hiyo hiyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: SAMATTA AENDELEA KUNG'ARA AFRIKA, AIPIGIA BAO MUHIMU UGENINI MAZEMBE CAF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top