• HABARI MPYA

  Ijumaa, Julai 26, 2013

  POULSEN AELEZEA MIKAKATI YA USHINDI NA UGANDA KESHO

  Na Mahmoud Zubeiry, Kampala, IMEWEKWA JULAI 26, 2013 SAA 7:00 MCHANA
  KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mdenmark, Kim Poulsen amesema katika mchezo wa kesho dhidi ya wenyeji, Uganda, The Cranes kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, hatakuwa na papara ya kupata bao la mapema, bali kucheza kwa nidhamu kujilinda wasifungwe bao na kuhakikisha wanapata mabao ndani ya dakika 90.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari katika hoteli ya Mt. Zion mjini hapa ambako imefikia Stars, Poulsen ameendelea kusistiza mchezo wa kesho utakuwa mgumu kwa sababu Uganda ni timu bora Afrika Mashariki, lakini amesema watapigania ushindi Uwanja wa Mandela, Namboole, kesho.

  Kocha Poulsen akizungumza na Waandishi wa Habari mchana wa leo Kampala. Kulia ni Msaidizi wake, Sylvester Marsh na kushoto ni Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura.

  Poulsen amesema itakuwa mbaya sana Cranes wakipata bao mapema, hivyo watacheza kwa nidhamu ya hali ya juu kuhakikisha hawaruhusu wapinzani wao hao kupata bao.
  Amesema maandalizi yalikuwa mazuri japokuwa atawakosa wachezaji fulani (Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta), kanunii haziwaruhusu kucheza CHAN kwa kuwa wanacheza nje ya Tanzania, klabu ya TP Mazembe ya DRC pamoja na viungo Mwinyi Kazimoto na Shomary Kapombe, ambao wamekwenda nje kufanya majaribio. Kazimoto amekwenda Qatar na Kapombe amekwenda Uholanzi.
  “Unapoingia katika mechi kama hizi lazima uwe umejiandaa kisaikolojia. Waganda wanajiamini kwa sbaabu walitufunga nyumbani na wamekuwa wakitamba kwamba watatufunga pia na hapa,”.
  “Ni muhimu kujua mabao yana maana makubwa, yanabadilisha mchezo na hali nzima, katika mechi ya kwanza tulitengeneza nafasi, tumejiandaa kutengeneza nafasi, na safari hii tutajitahidi kuzitumia kufunga. Tumefanya mazoezi ya namna ya kushambulia, namna ya kutengeneza nafasi, namna ya kwenda na namna ya kumalizia,”.
  “Na tumeona mazoezini kuna wachezaji ambao wanaweza kutumia nafasi kufunga, kwa sababu kitu kimoja, hakika tuko hapa kufunga, tunatakiwa kufunga, ili kusonga mbele kwenye mashindano. Pili tumefanyia mazoezi kujilinda.Mechi iliyopita, safu yetu ya ulinzi iliwapa nafasi chache wapinzani, si nafasi nyingi kwa Uganda,”.
  “Tunataka kuendelea na hilo na pia tunataka kutoruhusu bao, tuwe na safu imara ya ulinzi, tusiruhusu bao, tunatakiwa kukumbuka katika mchezo wa kesho, tuchukulie kama ni 0-0, hatuna haja ya kufunga katika dakika tano za mwanzo, kwa sababu tuna dakika 90, au zaidi za kufanya kazi,”.
  “Hivyo tunahitaji kucheza kwa nidhamu, ili kuwa katika uwiano mzuri, kwa sababu tunajua ndani ya dakika 90 tutatengeneza nafasi. Na nafasi zikipatikana ni juu ya nguvu ya kufunga mabao, kisha baada ya hapo, mchezo utabadilika,”.
  Poulsen amesema katika mchezo wa kesho, kulinganisha na mchezo wa kwanza, kutakuwa na mabadiliko katika kikosi cha kwanza, kutokana na kuondoka kwa Kazimoto na Kapombe, ambao walicheza mechi ya Dar es Salaam, Stars ikilala 1-0.
  Alisema hicho ni kiwango kidogo cha wachezaji na walijiandaa kwa hilo, kwa sababu walijua mapema watawakosa wachezaji hao.
  Kocha Poulsen akisom,a gazeti la Vission la Uganda lililoandika habari kuhusu mechi hiyo ya kesho


  Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura akimuambia jambo Kocha Poulsen wakati wa Mkutano

  Hakusema atapangaje kikosi chake, lakini inaonekana Juma Kaseja ataanza langoni, kulia David Luhende, kushoto Erasto Nyoni na katikati Aggrey Morris na Kevin Yondan, wakati viungo watakuwa Frank Domayo, Athumani Iddi ‘Chuji’, Salum Abubakar na Amri Kiemba huku washambuliaji wakiwa Mrisho Ngassa na John Bocco ‘Adebayor’.  
  Stars inatakiwa kushinda mabao 2-0 kesho ili kusonga mbele, baada ya kufungwa 1-0 wiki mbili zilizopita Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza, au kushinda 1-0 ili mchezo uamuliwe kwa mikwaju ya penalti
  Na timu ikiwa Mwanza katika kambi yake ya siku baada ya mechi ya kwanza kabla ya kuja hapa juzi, ilifanyia pia mazoezi na upigwaji wa penalti.
  Mchezo wa kesho utakuwa wa 15 kwa Poulsen, tangu aanze kazi Stars, akiwa ameshinda mechi tano, sare nne na kufungwa tano.
  Tanzania imewahi kushiriki Fainali za CHAN mara moja, mwaka 2009 nchini Ivory Coast ambazo zilikuwa za kwanza, wakati Uganda pia ilicheza mara moja mwaka 2011- hivyo zote zitakuwa zinawania nafasi ya pili kesho.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: POULSEN AELEZEA MIKAKATI YA USHINDI NA UGANDA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top