• HABARI MPYA

  Jumatano, Julai 24, 2013

  COASTAL UNION YAWACHAPA 1-0 WABABE WA SIMBA NA YANGA MKWAKWANI LEO

  Na Oscar Assenga,Tanga, IMEWEKWA JULAI 24, 2013 SAA 2:05 USIKU
  COASTAL Union ya Tanga imeonyesha iko sawa kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya jioni hii kuilaza 1-0 URA ya Uganda kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
  Shujaa wa Coastal jioni ya leo alikuwa ni mshambuliaji mpya, Keneth Masumbuko aliyesajiliwa kutoka Polisi Morogoro, ambaye alifunga bao hilo pekee la ushindi.
  Masumbuko alifunga bao hilo dakika ya 70, akiunganisha pasi ya Uhuru Suleiman aliyewatoka mabeki wa URA.
  Kwa ushindi huo, Coastal inayofundishwa na kocha Mzanzibari, Hemed Morocco imefanya kile ambacho vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga walishindwa mbele ya Watoza Kodi hao wa Uganda.
  Ameng'ara leo; Suleiman Kassim 'Selembe' ameng'ara leo Coastal ikiichapa URA 1-0 

  URA iliifunga Simba SC 2-1 kabla ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Yanga Uwanja wa Dar es Salaam wikiendi iliyopita.
  Mchezo huo ulikuwa na kasi ya vuta ni kuvute ambapo mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika hakuna timu iliyokuwa imeona lango la mwenzake, kipindi cha pili timu zote ziliingia uwanja hapo zikiwa na hari na nguvu ya kutaka kuibuka na ushindi.
  Kipindi cha pili Coastal Union walifanya mabadiliko yaliyoweza kuzaa matunda kwa kuwatoa Daniel Lyanga ambaye nafasi yake ilichukuliwa Selamani Kassim Selembe kwenye dakika ya 54 kuingia kwa mchezaji huyo kuliongeza nguvu ya mashambulizi na kuweza kufanikiwa kucheza nusu uwanja.
  Wachezaji wengine walioingia kipindi cha pili na kuongeza kasi ya mashambulizi yaliyofanikiwa kudhaa matunda ni Abdi Banda aliyechukua nafasi ya Othumani Tamim dakika 55 huku dakika moja baadae akatoka Hamadi Juma na kuingia Mbwana Kibacha mabadiliko hayoa yaliweza kuleta mafanikio makubwa hasa kwenye kikosi hicho ambacho kinajiandaa na Ligi kuu Tanzania bara.
  Wakionekana kucheza kwa kujipanga na kujituma, Coastal Union waliweza kufanya mashambulio ya mara kwa mara langoni mwa URA huku wachezaji wake wakipiga mashuti yaliyokuwa yakiupanguliwa na mlinda mlando wa URA Bwete Brian.
  Kutokana na mashambulio hayo Coastal Union waliweza nao kujipanga na kuweza kuthibiti vizuri safu yao ya ulinzi kwa kuwa makini na wachezaji wa URA hali ambayo iliwapa wakati mgumu kufika langoni mwa Coastal Union ambapo katika dakika ya 83 Coastal Union walifanya mabadiliko ya kumtoa Keneth Masumbuko na kumuingiza Pius Kisambale.
  Huku URA walifanya mabadiko kwenye dakika ya 84 wakimtoaWalulya Derrick na kumuingiza Lugya Ronald ambapo licha ya kucheza vema lakini walishindwa kubadilisha matokeo kwenye mechi hiyo ambayo ilikuwa na upinzani mkubwa kwa timu zote mbili.
  Wachezaji walioweza kuwakonga nyoyo vilivyo mashabiki wa Coastal Union ya Tanga ni Uhuru Selemani ambaye alikuwa mwiba kwa wachezaji wa Uganda huku mashabiki wa soka waliojitokeza kwenye mechi hiyo, wakimshangilia vilivyo kila alipokuwa akigusa mpira,huku wachezaji wengine akiwemo Juma Nyoso,Haruna Moshi "Boban"wakiwafurahisha mashabiki kwa kucheza soka nzuri .
  Kikosi cha Coastal Union leo kiliwakilishwa na mlinda mlango Shaban Kado,Hamad Juma,Othuman Tamim,Markus Ndehele,Juma Said "Nyoso"Jerry Santos,Uhuru Seleman,Crispian Odula,Daniel Lyanga,Haruna Moshi Boban na Keneth Masumbuko.
  Kwa upande wa URA waliwakilishwa na Bwete Brian, Walulya Derrick, Sekijo Samweli, Munaaba Allan, Docca Musa, Agaba Oscar, Nkugwe Elkamack, Feri Ally, Ngama Emanuel, Lutimba Yayo, Kasibante James, Mugabi Yasin, Ganya Willy na Lugya  Ronald.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: COASTAL UNION YAWACHAPA 1-0 WABABE WA SIMBA NA YANGA MKWAKWANI LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top