• HABARI MPYA

  Jumamosi, Julai 27, 2013

  KIIZA AREJEA TENA UGANDA BILA KUSAINI YANGA SC, BIN KLEB...

  Na Mahmoud Zubeiry, Kampala, IMEWEKWA JULAI 27, 2013 SAA 3:38 ASUBUHI
  SINEMA ya Yanga SC Hamisi Friday Kiiza ‘Diego’ inaendelea na sasa mchezaji huyo amerejea Uganda bila kusaini Mkataba mpya, ikiwa ni siku mbili tangu aambiwe arejee Dar es Salaam kusaini Mkataba wa miaka miwili kuendelea kupiga kazi Jangwani.
  Hii ni mara ya tatu, Yanga SC wanashindwa kumalizana na Kiiza baada ya kumuita mezani na hakuna uhakika kama kutakuwa na kikao kingine.
  Huyu vipi? Hamisi Kiiza akiwa amenyanyua Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu na Simon Msuva. Mchezaji huyo amerejea tena Uganda baada ya kushindwa kumalizana na Yanga SC

  Awali, mara tu baada ya Ligi Kuu, Yanga ilifanya mazungumzo na mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uganda, hawakufikika makubaliano akaondoka. Mara ya pili, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Mussa Katabaro akapanda ndege Uganda kuzungumza naye, wakafikia makubaliano akamtumia tiketi aende Dar es Salaam.
  Hata hivyo, mpachika mabao huyo alipofika Dar es Salaam akaona kama anapotezewa muda, kwa sababu Yanga ilionekana kutegeshea matokeo ya majaribio ya mshambuliaji kutoka Nigeria, Ogbu Brendan Chukwudi, akifuzu imteme Kiiza, na Mganda huyo akapanda ndege kurejea Kampala.
  Yanga SC baada ya kugundua Chukwudi ni majeruhi wa muda mrefu, ikamtumia tiketi Kiiza katikati ya wiki arejee Dar es Salaam, lakini jana kapanda ndege kurejea Uganda, bila kusiani Mkataba.
  Hii biashara vipi? Bin Kleb kulia akizungumza na Kiiza. Yanga SC kwa mara nyingine imeshindwa kumalizana na Kiiza na karejea Uganda.

  BIN ZUBEIRY ilimtafuta kwenye simu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga SC, Abdallah Ahmed Bin Kleb kuzungumzia hatima ya mchezaji huyo, lakini kwa bahati mbaya hakupokea siku.   
  Tayari mshambuliaji Mnigeria, Ogbu Brendan Chukwudi amerejeshwa kwao jana. 
  Lakini tayari Yanga imesajili mshambuliaji mwingine mzawa, Hussein Javu aliyesaini Mkataba wa miaka miwili kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro.
  Kusajiliwa kwa Javu, kunaongeza ushindani katika safu ya ushambuliaji ya Yanga SC, kwani sasa inakuwa na watu wanne, wengine ni Jerry Tegete, Didier Kavumbangu na Shaaban Kondo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: KIIZA AREJEA TENA UGANDA BILA KUSAINI YANGA SC, BIN KLEB... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top