• HABARI MPYA

  Jumanne, Julai 23, 2013

  SIMBA SC WAINGIA KAMBINI BAMBA BEACH KUJIANDAA KUIVAA TP MAZEMBE AGOSTI 8

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JULAI 23, 3013 SAA 3: 52 USIKU
  SIMBA SC leo imeingia kambini Bamba Beach Hotel, Kigamboni, Dar es Salaam kujiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inayotarajiwa kuanza Agosti 24, mwaka huu.
  Simba SC inayofundishwa na mchezaji wake wa zamani, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ itakuwa huko ikijifua vikali hadi itakapokuja mjini Agosti 8, kwa ajili ya kucheza mechi maalum katika Simba Day.
  Bado haijajulikana Simba SC itacheza na nani Agosti 8, lakini habari za ndani zinasema Wekundu hao wa Msimbazi wanaweza kucheza na mabingwa mara nne Afrika, TP Mazembe ya DRC.
  Kambini Bamba; Kikosi cha Simba kilichofungwa 2-1 na URA

  Maana yake- kama mechi hiyo itapatikana, mshambuliaji Mbwana Samatta wa Mazembe atacheza dhidi ya timu yake ya zamani kwa mara ya kwanza tangu ahamie DRC mwaka juzi.    
  Simba SC inaingia kambini baada ya Jumamosi kuchapwa mabao 2-1 na URA ya Uganda katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa Michael Magori aliyesaidiwa na Iddi Likongoti na Omar Mfaume wa Dar es Salaam, hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji mpya, Betram Mombeki aliyegongeana pasi vizuri na Marcel Boniventura. Mombeki alichukua pasi ya Singano ‘Messi’ akawapangua mabeki wa URA kabla ya kumpelekea pasi fupi Marcel aliyemrudishia mshambuliaji huyo mpya, akaunganisha nyavuni.
  Baada ya kufunga bao hilo, Mombeki alikwenda kushangilia kwa staili ya mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Nigeria, marehemu Rashid Yakini kwa kuingia kucheza ndani ya nyavu.  
  Enzi zake Msimbazi; Mbwana
  Samatta anaweza kuikabili timu
  yake ya zamani, SImba SC Agosti 8

  Kwa ujumla Simba SC ndio waliotawala mchezo kipindi cha kwanza wakionana vema na kucheza kwa kujiamini, wakati kwa URA iliwawia vigumu kuupenya ukuta wa Wekundu wa Msimbazi, uliokuwa chini ya Mganda mwenzao, Samuel Ssenkoom, ambaye ametemwa baada ya mechi hiyo.
  Kipindi cha pili, Simba SC inayofundiahwa na kocha mzalendo, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ ilirudi vizuri na kuendelea kuwapa raha mashabiki wake kwa soka maridadi. 
  Hata hivyo, kibao kiliigeukia Simba SC baada ya mshambuliaji wake, Mombeki kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kiwiko beki wa URA, Jonathan Mugabi dakika ya 51, ambaye alishindwa kuendelea na mchezo.
  Baada ya hapo kwa kuwa tayari mshambuliaji mwingine aliyekuwa akiisumbua ngome ya URA, Zahor Pazi alikuwa amekwishatolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Twaha Ibrahim, mabeki wa timu ya Uganda, wakiongozwa na Joseph Owino anayesajiliwa Simba SC baada ya mechi hiyo na Derick Walullya walianza kupanda zaidi kusaidia mashambulizi.
  URA ilipata bao lake la kusawazisha dakika ya 60 mfungaji Lutimba Yayo akiunganisha krosi nzuri ya Walullya.
  Wakati SImba wakijaribu kusaka bao la pili, Yayo tena akaifungia URA bao la ushindi dakika ya 75.  
  Hakukuwa tena na mashambulizi ya uhai kwa upande wa Simba na URA hawakuweza kumfunga Mganda mwenzao, Abbel Dhaira zaidi ya mara mbili. 
  Siku hiyo, kikosi cha Simba SC kilikuwa; Abbel Dhaira, Nassor Masoud ‘Chollo’, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Rahim Juma/Sino Augustino, Samuel Ssenkoom, Jonas Mkude, Ramadhani Singano/Miraj Adam, William Lucian, Betram Mombeki, Zahor Pazi/Twaha Ibrahim na Marcel Boniventura.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: SIMBA SC WAINGIA KAMBINI BAMBA BEACH KUJIANDAA KUIVAA TP MAZEMBE AGOSTI 8 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top