• HABARI MPYA

    Sunday, July 28, 2013

    HAKUKUWA NA GERVINHO WALA KALOU JANA, LAKINI…

    IMEWEKWA JULAI 28, 2013 SAA 2:05 ASUBUHI
    TANZANIA jana imetolewa katika michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, baada ya kufungwa na wenyeji Uganda mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa.
    Kwa matokeo hayo, Tanzania inayofundishwa na kocha Mdenmark, Kim Poulsen imetolewa kwa jumla ya mabao 4-1, baada ya wiki mbili zilizopita kufungwa 1-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

    Stars inatolewa kwenye CHAN ikiwa tayari imepoteza matumani ya kufuzu kwenye Fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil katika Kundi lake, D baada ya kufungwa mechi mbili mfululizo nyumbani na ugenini, 2-1 dhidi ya Morocco mjini Marakech na 4-2 dhidi ya Ivory Coast Dar es Salaam mwezi huu. 
    Aidha, huu unakuwa mchezo wa nne mfululizo Tanzania inafungwa- mbili ugenini wa leo na wa Morocco 2-1, Ivory na Coast na Uganda wiki mbili zilizopita.  
    Ikiwa ina mechi moja ya kukamilisha Ratiba katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil dhidi ya Gambia, Stars inatakiwa kujipanga kwa ajili ya mechi za kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika zinazotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu.  
    Mapema kabla ya mechi hiyo, ulitokea mgomo wa wachezaji kadhaa tegemeo, ambao ilibidi wabembelezwe hadi wakakubali kujiunga na timu kwa ajili ya mchezo wa jana.
    Poulsen alilazimika kufanya kazi kubwa kuwashawishi wachezaji kadhaa nyota kujiunga na timu kwa ajili ya mechi hiyo, wakiwemo viungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Athumani Iddi ‘Chuji’ na mshambuliaji, John Bocco ‘Adebayor’ ambao hawakutaka kwenda hata Mwanza, ambako Stars iliweka kambi ya siku 10 kujiandaa na mchezo huo, baada ya kufungwa 1-0 kwenye mchezo wa kwanza.
    Kocha Poulsen na Msaidizi wake, Sylvester Marsh waliwabembeleza mno wachezaji hao kupanda ndege kwenda Mwanza hadi wakakubali na kwa Bocco ilibidi apelekwe na Katibu wa klabu yake, Azam FC, Nassor Mohammed Idrisa ‘Father’ baada ya kugoma kabisa.
    Sure Boy alikuwa anakataa kwenda Mwanza akitoa sababu anaumwa, wakati Chuji alikuwa anakataa kwa sababu ya kuwekwa benchi Stars na Bocco hakutaja sababu.
    Chuji alikuwa hatumiwi na Poulsen Stars licha ya kuitwa mara zote na alikaa benchi kwa dakika zote 90 Stars ikilala 1-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Uganda na baada ya mechi hiyo akasema anajitoa kwa sababu umuhimu wake hauonekani katika timu hiyo ya nchi.
    Lakini kutokana na kiungo Mwinyi Kazimoto kutimkia Qatar, Poulsen akalazimika kumbembeleza Chuji abaki kikosini.
    Hata wakati timu ikiwa Mwanza, wachezaji hao wote walikuwa wanataka kugoma kuja Kampala na Poulsen na Marsh wakajitwisha jukumu lingine la kuwambeleza kupanda ndege kuja Uganda.
    Haijulikani haswa undani wa matatizo ya wachezaji hao, husuan Sure Boy ambaye ni kipenzi cha kocha huyo Mdenmark- lakini inawezekana matokeo mabaya katika mechi tatu zilizopita yanaweza kuchangia kuwashusha morali.
    Lakini pia, inaonekana Sure amechoka baada ya kucheza muda mrefu bila kupumzika na ndiyo maana anataka kupumzika. Msimu wa pili unaingia, Sure amekuwa akicheza kila mechi ya Stars na Azam FC tangu mwaka jana na anapokosekana, huwa mgonjwa hali ambayo haijatokea sana.
    Tuna tatizo la msingi katika soka yetu ambalo kama hatutalitazama kwa kina, tutaendelea kuwa wasindikizaji kwenye michuano.  Siku moja kabla ya mechi, nilimuuliza Poulsen juu ya kutokuwa na mabeki halisi wa pembeni katika timu yake na majibu yake nilithibitisha jana Namboole. 
    Kwanza Kim alisema amekuwa akiwaita mara kadhaa mabeki Wazanzibari, Nassor Masoud ‘Chollo’ na Waziri Salum, lakini wamekuwa wakitoa visingizio mara zote vya kuepuka kujiunga na timu hiyo na ndiyo maana akalazimika muda mrefu kumchezesha kiungo Shomary Kapombe katika nafasi hiyo, huku watu wakiamini anakosea kwa sababu nchi ina mabeki wengi wa pembeni.
    Alisema kila mara alipomuita Chollo wa Simba SC na Waziri wa Azam FC, zote za Dar es Salaam wamekuwa wakitoa udhuru- maana yake hawataki kuchezea timu ya taifa, naye ameona hana sababu ya kuendelea kuwalazimisha.
    Akasema nafasi ya beki wa pembeni ni ngumu na anahitaji kumuandaa mchezaji yeyote kabla ya kuanza kumtumia, ila kwa sasa kutokana na dharula amelazimika kumchukua David Luhende wa Yanga, ambaye alitarajia asingemuangusha.
    “Luhende akiwa anacheza Yanga anakuwa ana asilimia 60 ya kushambulia na 40 ya kuzuia. Sasa unapokuja timu ya taifa, inabadilika, kwa sababu unacheza mechi dhidi ya timu ngumu kama za Afrika Magharibi na kwingine katika nchi zilizoendelea. Huku (Stars) asilimia kubwa inakuwa kukaba,”alisema.
    “Huwezi kucheza dhidi ya mtu kama Gervinho au Solomon Kalou, halafu uwe unashambulia zaidi, lazima umdhbitii sana,”alisema. Hakukuwa na Gervinho wala Kalou jana Namboole, lakini Luhende alikuwa uchochoro na akasababisha penalti iliyoivurigia kabisa Stars hadi akatolewa na nafasi yake akamalizia winga Vincent Barnabas.
    Hakuna haja ya kumlaumu Luhende, bali inazungumziwa hali halisi kwamba ukitaka kuutathmini mchezo wa jana katika sababu za kufungwa, huwezi kukwepa kutaja jina la beki huyo Yanga SC- ambaye hata hivyo kwenye Ligi Kuu amekuwa akifanya vizuri.
    Siku zote watu wanakumbuka zamani, zama kwa zama. Wakati wa akina Peter Tino, watu walimkumbuka Maulid Dilunga (sasa marehemu). Wakati wa akina Innocent Haule alikumbukwa Tino. Wakati wa akina Nteze John, alikumbukwa Haule. Wakati wa akina Emmanuel Gabriel alikumbukwa Nteze na katika zama hizi za akina John Bocco, watu wanawakumbuka akina Gabriel. 
    Hiyo ndiyo imekuwa desturi yetu Watanzania- hatupendi kuweka mezani mijadala itakayoleta suluhisho la kweli juu ya matatizo ya kweli ya soka yetu. Dunia ya soka ya leo imebadilika, watu hawalaumiani, bali wanaambiana ili kujifundisha kwa kuwa soka ni mchezo wa makosa na vita ya kila timu ni kupambana kupunguza makosa.
    Timu yetu ina matatizo mengi- tulikuwa tunalia na washambuliaji wanapokosekana Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, lakini tumeona kumbe hata Sure Boy akiwa hayuko sawa, Frank Domayo akaumia- safu hiyo inakuwa lonya. Tulidhani tumemaliza tatizo la mabeki wa pembeni, lakini kumbe Chollo akisusa na Shomary Kapombe akakosekana, hali ni mbaya.
    Hatujajadili chochote kuhusu makipa wala mabeki wa kati- kwa sasa Yondan na Aggrey Morris wakisimama pamoja, kwenye benchi anabaki Nadir Cannavaro peke yake.
    Umefika wakati sasa tujitazame mara mbili- ni kweli nchi hii haina wachezaji au tunashindwa kuinua viwango vya wachezaji wetu? Tuna mashindano mengi ya vijana hivi sasa, ambayo yanasaidia kuzalisha vipaji vingi, lakini tunaviendelezaje? Tuna akademi ngapi zaidi ya ile ya Azam FC inayolea wachezaji katika misingi mizuri?
    Hakuna kocha mgeni ambaye amewahi kuwa mzuri kwetu, wote mwishowe huwa wanaondoka wakiwa hawana hamu tena na hii nchi. Tatizo liko wapi kama si sisi wenyewe- na haswa wale watu ambao wamepewa dhamana ya kuongoza soka yetu katika ngazi tofauti kuanzia ya klabu? 
    Tumekuwa watu wa kutamani vya wengine tu kila siku na hatuna kabisa mipango ya kutengeneza vya kwetu. Siku za mwanzoni za kuja kwangu Uganda, nilikuwa naulizwa kuhusu wachezaji wastaafu wa Tanzania- kama akina Zamoyoni Mogella na Edibily Lunyamila, lakini hadithi imebadilika, siku hizi nikija lazima niulize Emmanuel Okwi na Hamisi Kiiza.  Tumekosea wapi? Haya ndiyo maswali ya kujiuliza Watanzania. 
    Waswahili wanasema, kuchamba kwingi, mwishowe kushika kinyesi- tutaendelea kufikiria kubadilisha makocha hadi lini, badala ya kuangalia matatizo yetu ya msingi ili kuyatafutia ufumbuzi?
    Leo Simba SC pale wanahaha kutafuta mabeki na washambuliaji wa kigeni- wakati huo huo Azam FC beki na mshambuliaji wake tegemeo ni wageni, na Yanga SC nako inategemeoa mabeki na washambuliaji wa kigeni. Kwa kuzingatia hizi ndizo timu bora nchini, ambazo zinategemewa kutoa wachezaji wa timu ya taifa, ikiwa zenyewe zinategemea wageni, Taifa Stars itoe wapi wachezaji?  
    Ili kwenda peponi, lazima kufa kwanza zaidi ya hapo ni kujidanganya- Watanzania, kama tunataka kuwa na timu bora ya taifa, lazima tufumbie macho yote ya wenzetu na kuweka azimio la kuinua viwango vya wachezaji wetu kwanza, waje kuibeba soka yetu. 
    Niliwahi kuandika kuhusu athari za TFF kulegeza mkanda juu ya azimio la Bagamoyo kwamba kuanzia msimu ujao, klabu za Ligi Kuu zisisajili wachezaji wa kigeni zaidi ya watatu, lakini wakubwa wakapuuza na timu zimeruhusiwa kuendelea kusajili wachezaji watano, sasa timu ya taifa itapata wapi wachezaji bora, ikiwa klabu bora zinatumia wachezaji wa kigeni kwa asilimia 45 kikosini?
    Hao Waganda waliotunyanyasa Ligi yao inatawaliwa na Waganda, lakini sisi kwetu mfungaji bora anatoka Ivory Coast, anayemfuatia anatokea Burundi na Simba SC wamesajili mfungaji bora wa Burundi, maana yake ndoto za kuibua akina Mbwana Samatta wengine hazipo tena. Matatizo ni mengi katika soka yetu na kila siku tumekuwa tukiyajadili, ila kwa saasa ni hili. Ramadhan Kareem. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: HAKUKUWA NA GERVINHO WALA KALOU JANA, LAKINI… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top