• HABARI MPYA

  Jumapili, Julai 21, 2013

  ASHANTI UNITED WAENDA 'BRAZIL' KUJIPANGA KWA LIGI KUU

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JULAI 21, 2013 SAA 6:04 MCHANA
  ASHANTI United ‘Watoto wa Mji’ ukipenda waite City Boys wanatarajiwa kufanya ziara mkoani Kigoma, maarufu kama Brazil ya Tanzania kujiandaa na msimu, mara tu baada ya kurejea Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Kigoma inaitwa Brazil ya Tanzania kwa sababu ya kuibua nyota wengi wa soka, kuanzia enzi za akina Sunday Manara, Athumani Juma Kalomba (marehemu), Abedi Mziba, hadi sasa akia Juma Kaseja.
  Ashanti itaondoka Dar es Salaam Jumanne na itakuwa Kigoma kwa takriban wiki mbili ikijifua na kucheza mechi za kujipima nguvu na timu mbalimbali za huko.
  Timu hiyo iliyorejea Ligi Kuu msimu huu, imekuwa ikijifua mjini Dar es Salaam kwa takriban mwezi mzima na kucheza mechi kadhaa za kujipima nguvu.
  Watoto wa Jiji; Wachezaji wa Ashanti wakisherehekea baada ya kurejea Ligi Kuu

  Mechi ya mwisho ilifungwa na Azam FC mabao 5-1 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na sasa inakwenda kurekebisha makosa Kigoma.
  Ashanti inakumbukwa enzi zake ikicheza Ligi Kuu muongo uliopita kwa kuibua vipaji vya nyota wengi ambao baadaye walikuwa tegemeo la timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
  Miongoni mwao ni kipa Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Juma Jabu, Juma Nyosso, Said Mourad, viungo Jabir Aziz, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ na wengineo.
  Timu hiyo yenye maskani yake katika soko la Ilala Boma, karibu kabisa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam inatarajiwa kuleta changamoto mpya katika Ligi Kuu, hususan dhidi ya timu kongwe, Simba na Yanga.
  Pamoja na kupandishwa Ligi Kuu na vijana wadogo wenye vipaji, Ashanti imejiimarisha kwa kuongeza wakongwe kadhaa, akiwemo mshambuliaji wa zamani wa Simba na Yanga, Said Maulid ‘SMG’ aliyekuwa anacheza Angola.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: ASHANTI UNITED WAENDA 'BRAZIL' KUJIPANGA KWA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top