• HABARI MPYA

  Ijumaa, Julai 26, 2013

  CHOLLO NA BEKI WA AZAM WAMEITWA MARA KADHAA STARS WANAGOMA, ALALAMIKA KOCHA

  Na Mahmoud Zubeiry, Kampala, IMEWEKWA JULAI 26, 2013 SAA 7:00 MCHANA
  KOCHA wa Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mdenmark, Kim Poulsen amesema kwamba amekuwa akiwaita mara kadhaa mabeki Wazanzibari, Nassor Masoud ‘Chollo’ na Waziri Salum, lakini wamekuwa wakitoa visingizio mara zote vya kuepuka kujiunga na timu hiyo.
  Poulsen alikuwa akizungumzia sababu ya kutokuwa na mabeki wengi wa pembeni katika kikosi chake, na pia muda mwingi akimchezesha kiungo Shomary Kapombe katika nafasi hiyo, wakati nchi ina mabeki wengi wa pembeni.
  Amesema kila mara anapomuita Chollo wa Simba SC na Waziri wa Azam FC, zote za Dar es Salaam wamekuwa wakitoa udhuru- maana yake hawataki kuchezea timu ya taifa, naye ameona hana sababu ya kuendelea kuwalazimisha.


  Amesema nafasi ya beki wa pembeni ni ngumu na anahitaji kumuandaa mchezaji yeyote kabla ya kuanza kumtumia, ila kwa sasa kutokana na dharula amelazimika kumchukua David Luhende wa Yanga, ambaye amemtengeneza na yuko tayari.
  “Luhende akiwa anacheza Yanga anakuwa ana asilimia 60 ya kushambulia na 40 ya kuzuia. Sasa unapokuja timu ya taifa, inabadilika, kwa sababu unacheza mechi dhidi ya timu ngumu kama za Afrika Magharibi na kwingine katika nchi zilizoendelea.
  Huku (Stars) asilimia kubwa inakuwa kukaba,”alisema.
  “Huwezi kucheza dhidi ya mtu kama Gervinho au Solomon Kalou, halafu uwe unashambulia zaidi, lazima umdhbitii sana,”alisema.
  Pamoja na hayo, Poulsen amemsifu Luhende kwamba ametumia muda mfupi kuelewa mfumo wa uchezaji wa Stars na ana matumaini naye makubwa katika mchezo wa kesho. 
  Stars kesho inamenyana na wenyeji, Uganda, The Cranes kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala.
  Katika mchezo huo, Stars inahitaji kushinda 2-0 ili kusonga mbele, baada ya kufungwa 1-0 katika mchezo wa kwanza mjini Dar es Salaam, au kushinda 1-0 na kisha mchezo uamuliwe kwa mikwaju ya penalti
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: CHOLLO NA BEKI WA AZAM WAMEITWA MARA KADHAA STARS WANAGOMA, ALALAMIKA KOCHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top