• HABARI MPYA

  Alhamisi, Julai 25, 2013

  WACHEZAJI STARS WALALAMIKIA FUTARI MBOVU HOTELINI KAMPALA

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JULAI 25, 2013 SAA 2:51 USIKU
  WACHEZAJI waislamu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars wamelalamikia futari ya chini ya kiwango wanayopatiwa katika hoteli ya Mt. Zion iliyopo mjini Kampala Uganda na jioni hii wamejikuta wakicheleweshwa kufuturu kwa takriban saa nzima.
  Stars imefikia katika hoteli hiyo tangu jana kwa ajili ya mechi dhidi ya wenyeji, Uganda keshokutwa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.
  Huu si uungwana; Chuji amelalamikia futari iliyo chini ya kiwango na wanayocheleweshewa hoteli ya Mt. Zion hapa Kampala

  BIN ZUBEIRY ilikuwepo katika hoteli hiyo tangu saa 10:30 jioni ili kujua maendeleo ya wachezaji na timu kwa ujumla na ulipowadia muda wa kufuturu, ndipo wachezaji walikutana na zahama hiyo.
  Kiungo tegemeo wa Stars, Athumani Iddi ‘Chuji’ alimuuliza muhusika wa hoteli hiyo juu ya kuwapatia chakula cha chini ya kiwango na ambacho kipo kinyume cha maelekezo au maombi yao, lakini hakuwa na majibu mazuri, hadi Mkuu wa Msafara, Ahmed ‘Msafiri’ Mgoyi alipoingilia kati. 
  Chuji alisema tangu jana wamekuwa wakipatiwa chakula kiliocho chini ya kiwango na pia kilicho kinyume na maombi yao. “Wewe jana umechukua oda ya vyakula tunavyotaka, lakini matokeo yake hapa tunajionea mambo tofauti, huu si uungwana, sisi tupo katika ibada ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan. Kutufanyia hivi unapata dhambi,”alisema Chuji.
  Meneja wa timu, Leopold Mukebezi ‘Tasso’ naye alilalamikia hali hiyo na akasema bila shaka wanafanyiwa hivyo kama mbinu za wenyeji kuwadhoofisha kuelekea mchezo wa keshokutwa.
  Wakati yote hayo yanaendelea, kocha Mkuu wa Stars, Mdenmark Kim Poulsen alikuwa ameketi na Wasaidizi wake, Sylvester Marsh, Jacob Michelsen na Juma Pondamali katika eneo la kuangalia Televisheni. Wachezaji waislamu waliokumbana na adha hiyo ni makipa Juma Kaseja, Mwadini Ali na Ali Mustafa ‘Barthez’, beki Nadir Haroub, viungo Amri Kiemba, Athuman Idd, Haroun Chanongo, Khamis Mcha, Mudhathir Yahya, Salum Abubakar na washambuliaji Juma Luizio na Mrisho Ngassa.
  Wachezaji wengine wa Stars wasio waislamu waliopo hapa ni mabeki Aggrey Morris, David Luhende, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani na Vincent Barnabas, viungo Frank Domayo na Simon Msuva na mshambuliaji John Bocco ‘Adebayor’.
  Stars iliwasili Kampala jana jioni tayari kwa mechi ya kuwania tiketi ya CHAN, Fainali ambazo zitafanyika mwakani nchini Afrika Kusini, ikitokea mini Mwanza ilipokuwa imepiga kambi ya siku kumi kujiandaa kwa mechi hiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya hizo mbili itakwenda Afrika Kusini.
  Stars leo haikufanya mazoezi kulingana na programu ya kocha Poulsen, lakini kesho itajifua kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole ambako mechi itapigwa keshokutwa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: WACHEZAJI STARS WALALAMIKIA FUTARI MBOVU HOTELINI KAMPALA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top