• HABARI MPYA

  Ijumaa, Julai 26, 2013

  IMEGUNDULIKA; SURE BOY, BOCCO CHUPUCHUPU KUJITOA STARS

  Na Mahmoud Zubeiry, Kampala, IMEWEKWA JULAI 26, 2013 SAA 4:09 USIKU
  WAKATI timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, inashuka dimbani kesho kumenyana na wenyeji, Uganda, The Cranes kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, kocha Mdenmark, Kim Poulsen alilazimika kufanya kazi kubwa kuwashawishi wachezaji kadhaa nyota kujiunga na timu kwa ajili ya mechi hiyo.
  BIN ZUBEIRY inafahamu wachezaji kadhaa nyota, wakiwemo viungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Athumani Iddi ‘Chuji’ na mshambuliaji, John Bocco ‘Adebayor’ hawakutaka kwenda hata Mwanza, ambako Stars iliweka kambi ya siku 10 kujiandaa na mchezo huo, baada ya kufungwa 1-0 kwenye mchezo wa kwanza.
  Hakutaka kuja; John Bocco 'Adebayor' hakutaka kuja Kampala

  Kocha Poulsen na Msaidizi wake, Sylvester Marsh waliwabembeleza mno wachezaji hao kupanda ndege kwenda Mwanza hadi wakakubali na kwa Bocco ilibidi apelekwe na Katibu wa klabu yake, Azam FC, Nassor Mohammed Idrisa ‘Father’ baada ya kugoma kabisa.
  Sure Boy alikuwa anakataa kwenda Mwanza kwa sababu anaumwa, wakati Chuji alikuwa anakataa kwa sababu ya kuwekwa benchi Stars na Bocco hakutaja sababu.
  Chuji alikuwa hatumiwi na Poulsen Stars licha ya kuitwa mara zote na alikaa benchi kwa dakika zote 90 Stars ikilala 1-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Uganda na baada ya mechi hiyo akasema anajitoa kwa sababu umuhimu wake hauonekani katika timu hiyo ya nchi.
  Lakini kutokana na kiungo Mwinyi Kazimoto kutimkia Qatar, Poulsen akalazimika kumbembeleza Chuji abaki kikosini.
  Hata wakati timu ikiwa Mwanza, wachezaji hao wote walikuwa wanataka kugoma kuja Kampala na Poulsen na Marsh wakajitwisha jukumu lingine la kuwambeleza kupanda ndege kuja Uganda.
  Anaumwa; Sure alisema anaumwa
  hakutaka kuja Kampala

  Haijulikani haswa undani wa matatizo ya wachezaji hao, husuan Sure Boy ambaye ni kipenzi cha kocha huyo Mdenmark- lakini inawezekana matokeo mabaya katika mechi tatu zilizopita yanaweza kuchangia kuwashusha morali.
  Lakini pia, inaonekana Sure amechoka baada ya kucheza muda mrefu bila kupumzika na ndiyo maana anataka kupumzika. Sure amekuwa akicheza kila mechi ya Stars na Azam FC tangu mwaka jana na anapokosekana, huwa mgonjwa hali ambayo haijatokea sana.
  Stars itashuka dimbani kesho Uwanja wa Mandela mjini hapa, ikitoka kufungwa mechi tatu mfululizo zilizopita, mbili kati ya hizo dhidi ya Ivory Coast 4-2 na Uganda 1-0 ikifungwa nyumbani Dar es Salaam, baada ya kufungwa 2-1 mjini Marakech na wenyeji Morocco.
  Awali ya hapo, Stars ilikuwa na mwenendo mzuri, ikishinda mechi tano mfululizo nyumbani kuanzia na Kenya (1-0), Zambia (1-0), Gambia (2-1), Cameroon (1-0) na Morocco (3-1)     
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: IMEGUNDULIKA; SURE BOY, BOCCO CHUPUCHUPU KUJITOA STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top