• HABARI MPYA

  Jumamosi, Julai 27, 2013

  KAMA TIMU ILIKUWA FEKI NA MCHEZAJI NAYE KWA NINI ASIWE FEKI?

  IMEWEKWA JULAI 27, 2013 SAA 2:53 ASUBUHI 
  KWA kupitia vyombo vya habari vya Tanzania na kwenye mitadao ya kijamii, tulitangaziwa timu ya Yanga imepata mshambuliaji hatari wa kimataifa, Ogbu Brendan Chukwudi kutoka timu ya Heartland ya Nigeria, inayochaza ligi kuu ya huko, anayesifika kwa upachikaji wa mabao. Chukwudi alitua usiku wa manane katika uwanja wa Ndege kimataifa wa Mwalimu Jk Nyerere akipokelewa na maofisa wa Yanga na kuwekwa chini ya ulinzi mkali sana wa vijana waaminifu wa Yanga, wakipeana zamu za ulinzi na iliripotiwa pia wakati mwingine alihamishwa hoteli kwa kuwahofia watani wao, Simba. Walidhani Simba wanataka na kumsainisha kama wanavyofanya wao wanapomtaka mchezaji aliyetakiwa na Simba- kwa kweli Yanga huwazidi wenzao maarifa mara nyingi mno.

  Leo hii  tunasikia tena Yanga hawataki hata kumsikia na tangu alivyoumia Uwanja wa Taifa siku ya mchezo wa kirafiki, eti hakuna kiongozi tena wa Yanga aliyemuona au kuonana naye achilia mbali kumjulia hali, anaendeleaje, mipango labda ya hospitali na kadhalika.
  Naye kupitia magazeti ameonekana kulalamika juu ya hilo la kutokutembelewa na viongozi na amebaki njia panda kama wana mtaka au la na kadai eti, kama Simba watamuihitaji yupo tayari kufanya nao kazi iwapo watafikia makubaliano ila kwa utata wa afya ya mchezaji walioiona nadhani nao hawana haja naye.
  Hapa napo kuna funzo kubwa sana kwa timu zetu za Tanzania, kuendesha vilabu vyetu kitaalamu, kikanuni, kitaratibu na kikatiba. Jamani kumbukeni sasa tupo kwenye soka la kulipwa si la Ridhaa tena. Sina hakika hata wakala alieyemleta anatambulika na FIFA- nina shaka na anaweza naye akawa feki, kwa sababu mawakala nao wana miiko yao ndio maana mtihani hutungwa na FIFA na kusimamiwa na Chama cha Mpira wa Miguu cha nchi husika kwa ajili yao wafaulu, wapewe uwakala.
  Ni aibu kubwa sana kwa viongozi wetu kutaka kucheza na timu FEKI, tena hawana hata kibali cha chama cho cha mpira wa miguu, hii ni hatari mno hata kwa wachezaji wetu kupata majeraha yasiyo na ulazima na timu kuingia gharama ya kuwauguza, achilia mbali kuikosa huduma ya mchezaji wake.
  Maana yake tunaelezwa nia yao ni kutafuta timu za kusajiliwa bahati mbaya kwao "DILI" LIMEBUMBULUKA kabla ya mipango yao kutimia, hongera sana TFF kwa umakini mliouonyesha kwa hili.
  Kuna kipindi  nafikiri ni mwaka juzi, sikumbuki vizuri alikuja mtu mmoja kutoka Zambia au Malawi, sina hakika sana, eti katoka katika kambuni ya Adidas wakaingia mkataba na timu ya Simba  na Yanga mbele ya Waandishi wa Habari kwa mbwembwe nyingi sana, lakini hadi leo hajaonekana tena.
  Inakuwaje timu kubwa wakati mwingine zinaongozwa na wanasheria zinashindwa kuwa makini? Kwanini wasijiridhishe kwanza , si kwa maneno ya muhusika, bali kwenda hata kuangalia biashara yenyewe na Ofisi hata kupitia mitandaoni, kampuni makini ya kimataifa utaikuta tu.
  Huyu anasema ni wakala, muombeni leseni, ingieni naye mkataba wa kuwauzia wachezaji sambamba na nakala ya leseni na paipoti yake, sasa hivi unaona kuna kashifa za madawa ya kulevya, wamekamatwa kwako wanadai ni mawakala, walete vielelezo, hawana wapelekwa Segerea.
  Kisa tu kufanyakazi kienyeji, pia historia yake ni namna nyingine ya kumjua mtu feki au la, kafanya kazi wapi na nani, mtawatafuta mtawauliza kama wanamjua kupitia mitandao tu, huhitaji gharama au simu, hiyo ndio kazi ya kitengo cha habari.
  Kuna uhuni mno katika biashara ya wachezaji, kama kuuzwa kwa Emanuel Okwi wa Simba kwenda Etoile du Sahel ya Tunisia, hata haijulikani kama ni kuuzwa, mkopo, bure ni huru. Unakwenda kushitaki FIFA kumbe hata wakala mwenyewe feki, utapoteza uhalali wa kusikilizwa kwa kesi yao.
  Kumbe yaelekea siku aliyokuja huyu mshamuliaji, nyuma yake wametua na wachezaji wengine 15 na viongozi wawili bila utambulisho kwa Waandashi wa Habari kama ilitokea, sijasikia basi niwatake Radhi ila ilikuja tu kuibuka Yanga kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa na Three Piller, timu mpya kutoka Nigeria iliyopanda daraja msimu huu.
  Imefikia Magomeni ikiwa na wachezaji 15 na viongozi wawili- nilijaribu kuwasiliana na wanamichezo wenzangu, kwa kweli wengi wetu tulitilia shaka timu inayocheza ligi kuu iende ugenini na wachezaji 15 na kufikia gesti ya uchochoroni.
  Tukawa na wasiwasi mkubwa mno juu ya uhalali wa timu hiyo, ila kuna mwanamichezo mwenzangu kutoka Morogoro jina namhifadhi, alisema tatizo la Watanzania, wamezoea msululu wa viongozi na mambo makubwa, nashukuru haikupita muda kupitia TFF wakathibitisha timu ni Feki. Na kwa kuwa wakala ni mmoja aliyeileta timu Feki, kwa nini mchezaji naye asiwe Feki au magumashi?
  Video yenyewe yatuonyesha akifunga magoli katika msimu mmoja tu na timu moja wakati kupita vyombo vya habari, amechezea zaidi ya timu tatu ambazo ni Unth alipoanzia soka la ushindani baadaye alihamia Enungu Rangers halafu Heartland alipochaguliwa katika timu ya Taifa.
  Kama hakupangwa, basi tungeona video akishiriki katika mazoezi, maana yake Nigeria ni timu ya vipaji vingi mno na wengi wanacheza nje, hadi inamuwia vigumu kocha kuchagua wachezaji, nani amwache na nani amchukue kama alipata nafasi hiyo basi hata mkanda akifanya mazoezi.
  Sina shaka kabisa na ile video kuwa ni yeye na ni kweli alionyesha uwezo wa kufunga magoli, viongizi kama wapo makini, hawawezi kudanganyika na video ya 2010/2011 tu, hapa katikati vipi?
  Na hakuna timu makini ya kumchukua mchezaji majeruhi, eti imtibu ianze kumtumia akipona, labda aumie amesajiliwa kama itatokea hivyo basi ni jambo jipya kwa soka la Tanzania.
  Kingine, ni vizuri kuwapima wachezaji hasa wa kutoka nje tunaotaka kuwasajili kuwachunguza zaidi hadi kujiridhisha kabla ya kuwaita- hakuna sababu ya uharaka.
  Si kwa Yanga na Simba, bali hata kwa vilabu vyota vya Tanzania, kuepuka gharama kwa timu zisizokuwa za lazima kama Yanga hivi sasa, wakati mwingine yanaweza kutokea hata maafa kama wana maradhi ya moyo na kadhalika.
  Mwisho, nawashauri viongazi wa vilabu vyetu tushindane kimaendelea zaidi si kimajina, tusiangalie mchezaji anatoka wapi, kuna kipindi Man U ya Uingereza ilikuwa na wachazaji kutoka visiwa Trinbad&Tobacco Dwight York na aliipa mafanikio sana sana timu, si lazima Nigeria, Cameroon na Ivory Cost.
  Sisi tunawadharau wachezaji wetu na hatuwapi mishahara mizuri wala huduma ni duni hadi vifaa usafiri na mahitaji mengi ili mchezaji awe fiti, wakati leo Samatta ni tegemeo TP Mazembe, isitoshe angekuwa Simba angekuwa kafungiwa fungiwa na kutupiwa vilago kama wenzake Kaseja, Nyoso, Maftah, Boban na wengine.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: KAMA TIMU ILIKUWA FEKI NA MCHEZAJI NAYE KWA NINI ASIWE FEKI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top