• HABARI MPYA

    Friday, July 19, 2013

    KOCHA BRANDTS ASEMA MSHAMBULIAJI MNIGERIA HAYUKO FITI, ANAHITAJI MUDA KUTHIBITISHA UWEZO

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JULAI 19, 2013 SAA 6:45 MCHANA
    KOCHA wa Yanga SC, Mholanzi Ernie Brandts amesema kwamba mshambuliaji Mnigeria, Ogbu Brendan Chukwudi amekuja akiwa majeruhi na ambaye hana mazoezi, hivyo hayuko fiti.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo, beki huyo wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi, amesema kwamba anampa muda mchezaji huyo ili awe sawa na kuthibitisha uwezo wake, kabla hajaupa baraka uongozi uingie naye mkataba.
    “Ni majeruhi, na ameniambia hajafanya mazoezi kwa muda, siwezi kusema chochote kuhusu yeye kwa sasa, ila Jumapili tunacheza mechi, nitampa nafasi, njoo umuone na wewe,”alisema. 
    Hayuko fiti; Mshambuliaji Ogbu Brendan Chukwudi amefika Yanga akiwa majeruhi na hayuko fiti

    Yanga ilimleta mchezaji huyo wa Heartland FC ya Nigeria mapema wiki hii (usiku wa kuamkia Jumanne) baada ya wapinzani wao, Simba SC kumsaini mfungaji wa bora wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Amisi Tambwe wa Vital’O ya Burundi.
    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20, aliiambia BIN ZUBEIRY kwamba msimu uliopita alifunga mabao 14 katika Ligi Kuu ya Nigeria na mwaka jana aliitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Nigeria, Super Eagles, lakini hakupata nafasi ya kucheza kutokana na wachezaji wa Ulaya kupewa nafasi zaidi.
    Alisema kabla ya kuja Yanga, alikuwa Misri ambako aliitwa na klabu moja iliyotaka kumsajili, lakini kutokana na vurugu za kisiasa zinazoendelea nchini humo sasa akaamua kuondoka kuja Tanzania kufuata wito wa Yanga SC.
    Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga SC, Abdallah Bin Kleb naye aliiambia BIN ZUBEIRY kwamba mchezaji huyo wamekuwa wakimfuatilia kwa muda mrefu na hadi kumleta nchini wameridhika naye ni bora.
    “Huyu ni bora, anajua kufunga, ni kijana mdogo na uwezo mkubwa sana. Aliitwa timu ya taifa ya Nigeria, kitu ambacho kwa nchi kama ile yenye wachezaji wengi wazuri kinaashiria huyu ni mchezaji mzuri sana,”alisema.
    Kleb alisema kwamba awali walikata tamaa ya kumpata mchezaji huyo baada ya kuitiwa dau nono Misri, lakini imekuwa bahati yao amekwepa machafuko huko na kuamua kuja kufanya kazi Tanzania.  
    Kleb alisema watamkabidhi kwa kocha Mholanzi, Ernie Brandts mchezaji huyo kabla ya kusaini naye Mkataba ili amuone na kutoa baraka zake.
    Anampa muda; Kocha Ernie Brandts amesema anampa muda Chukwudi ili athibitishe uwezo, ndipo apendekeza usajili wake

    Nchini Nigeria, vyombo vya habari vinamsifu Brendan kama mshambuliaji kinda mwenye nguvu, kasi, uwezo wa hali ya juu na ufundi pia. Klabu ya Esperance Sportif ya Tunisia ilijaribu kumsajili msimu huu kujiongezea nguvu katika kampeni zake za kuwania taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini pande hizo mbili zikashindwa kufikia makualiano.
    Ni hatari mno anapoingia kwenye eneo la hatari na ana kipaji cha hali ya juu cha kufunga kwa kichwa na miguu yote- na ni mmaliziaji mzuri.
    Mshambuliaji huyo alijiunga na Heartland msimu uliopita akitokea Enugu Rangers, aliyoanza kuichezea mwaka 2008. Kisoka Ogbu aliibukia Unth Enugu, kabla hajajiunga na Enugu Rangers.
    Brendan aliifungia mabao 11 Enugu Rangers na kuwa mfungaji bora wa klabu katika Ligi Kuu msimu wa 2010/2011 na akaihama klabu hiyo, akiwa ameifungia jumla ya mabao 30 kwenye mashindano yote.
    Alikuwa miongoni mwa wachezaji wapya walioitwa na kocha Stephen Keshi katika kikosi cha Nigeria, kiliochokwenda kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Afrika Kusini pamoja na Tony Okpotu wa Lobi Stars, Mannir Ubale wa Kano Pillars na Fidelis Saviour, aliyekuwa FC Taraba kabla ya kuhamia Enyimba. 
    Kama atasajiliwa Yanga, Ogbu atakamilisha idadi ya wachezaji watano wa kigeni wanaotakiwa kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu, wengine wakiwa ni beki Mbuyu Twite (Rwanda), kiungo Haruna Niyonzima (Rwanda) na washambuliaji Didier Kavumbangu (Burundi) na Hamisi Kiiza (Uganda).
    Lakini Kiiza amemaliza Mkataba wake Yanga, ingawa ameitwa na tayari yupo nchini kwa ajili ya kuonegza Mkataba.
    Chukwudi anaweza kuwa kiu ya jibu kwa mashabiki wa Yanga juu ya safu yao ya ushambuliaji- baada ya kuonekana wazi msimu uliopita inahitaji mkali wa aina yake, kutokana na wachezaji waliopo sasa kushindwa kuichumia klabu mabao ya kutosha.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KOCHA BRANDTS ASEMA MSHAMBULIAJI MNIGERIA HAYUKO FITI, ANAHITAJI MUDA KUTHIBITISHA UWEZO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top