• HABARI MPYA

    Sunday, July 21, 2013

    REFA WA MADAGASCAR ABEBA HATIMA YA STARS CHAN DHIDI YA UGANDA

    Na Boniface Wambura, IMEWEKWA JULAI 21, 2013 SAA 5:40 ASUBUHI
    SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Madagascar kuchezesha mechi kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Uganda (The Cranes) itakayochezwa Jumamosi (Julai 27 mwaka huu) Uwanja wa Mandela ulioko Namboole nje kidogo ya Jiji la Kampala.
    Waamuzi wataongozwa na Kanoso Abdoul Ohabee wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Andirvoavonjy Pierre Jean Eric. Mwamuzi msaidizi namba mbili ni Jinoro Velomanana Ferdinand huku Andriamiharisoa Hubert Marie Bruno akiwa mwamuzi wa mezani (fourth official).
    Askari wetu; Kikosi cha Stars kilichofungwa 1-0 na Uganda Dar es Salaam. Kitapanda mlima Kampala?

    Kamishna wa mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya mwisho kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) ni Ismail Kamal kutoka Ethiopia.
    Mechi hiyo namba 38 itachezwa kuanzia saa 10 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki. Taifa Stars ilipoteza mechi ya kwanza iliyochezwa Julai 13 mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa bao 1-0.
    Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iko kambini jijini Mwanza ikijiandaa kwa mechi hiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya hizo mbili itacheza Fainali za CHAN mwakani nchini Afrika Kusini.
    Katika mchezo wa kwanza baina ya timu hizo, Stars ilichapwa bao 1-0 Dennis Iguma dakika ya 46.
    Iguma aliifungia The Cranes bao hilo, baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Stars kufuatia krosi maridadi ya Brian Majwega, ambaye leo alikuwa mwiba mkali kwa Taifa Stars. 
    Hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na kwa ujumla katika dakika zote hizo 45 hakukuwa na shambulizi la kutisha kwa pande zote.
    Brian Majwega alifanikiwa kumgeuza uchochoro Erasto Nyoni na kuingia ndani mara kadhaa, lakini pasi na krosi zake ziliokolewa na mabeki wa Stars inayofundishwa na Mdenmark, Kim Poulsen.
    Mrisho Ngassa alipewa mipira mirefu kadhaa, lakini mabeki wa Uganda wakiongozwa na mkongwe, Nahodha wao, Hassan Wasswa walisimama imara kumdhibiti.
    Mashambulizi mengine ya Stars yalipitia kwa John Bocco ‘Adebayor’, ambaye alikuwa anapigiwa mipira mirefu, lakini alidhibitiwa pia. Timu zote zilicheza sawa kipindi cha kwanza. 
    Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko, Stars ikiwapumzisha beki Erasto Nyoni na kiungo Mwinyi Kazimoto na kuwaingiza David Luhende na Haroun Chanongo, lakini walikuwa ni Uganda wanaofundishwa na makocha wa zamani wa klabu ya Yanga, Mserbia Milutin Sredojevic ‘Micho’ anayesaidiwa na Sam Timbe waliobuka vinara.  
    Lakini baada ya kufungwa Stars, waliongeza kasi na nguvu ya uchezaji na kufanikiwa tu kulitia misukosuko lango la Uganda na si kupata bao japo la kusawazisha.
    Matokeo hayo yanamaanisha Stars itahitaji kushinda ugenini kuanzia mabao 2-0 wikiendi ijayo ili isonge mbele, vinginevyo itakuwa imetupwa nje ya mashindano hayo.
    Stars itawakosa viungo wa Simba SC, Shomary Kapombe aliyekwenda Uholanzi na Mwinyi Kazimoto aliyekwenda Qatar, wote kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa. 
    Wachezaji walioko kambini katika kikosi cha Stars mjini Mwanza ni Juma Kaseja, Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vincent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd na Haruni Chanongo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: REFA WA MADAGASCAR ABEBA HATIMA YA STARS CHAN DHIDI YA UGANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top