• HABARI MPYA

    Saturday, July 20, 2013

    KIIZA AWAACHA UCHOCHORONI YANGA, APANDA KQ KUREJEA KAMPALA BAADA YA JANA KUFANYA MAZOEZI NA URA

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JULAI 20, 2013 SAA 4:45 ASUBUHI
    HAMISI Friday Kiiza jana alifanya mazoezi na URA ya Uganda Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikijiandaa na kucheza na Simba SC leo- na leo asubuhi majira ya saa 4:25 amepanda ndege ya KQ kurejea Kampala akiachana na mpango wa kusaini Mkataba Yanga SC.
    Baada ya kumaliza Mkataba wake wa awali wa miaka miwili na Yanga SC, Kiiza ameingia kwenye mvutano na viongozi wa klabu hiyo juu ya Mkataba mpya na awali aliachana nao na kurejea Kampala, wakamfuata kwa mazungumzo na baadaye wakamtumia tiketi akarejea Dar es Salaam.
    Amewashitukia; Kiiza kulia akiwa na kigogo wa usajili wa Yanga SC, Seif Ahmad 'Magari', mchezaji huyo ameondoka leo baada ya kushitukia Yanga wanataka kumpotezea muda akose timu

    Lakini baada ya wiki moja, Kiiza anarejea Dar es Salaam akiwa hajasaini na habari zinasema alikuwa anazungushwa, kila siku akipewa dola za Kimarekani 35 za kwenda kubadilisha tarehe ya kuondoka, huku akipewa Sh. 50,000 za matumizi kila siku.
    Lakini kutokana na kuvuja kwa habari kwamba, Yanga SC inataka mshambuliaji mwingine mzuri zaidi ili iachane na Kiiza, Mganda huyo maarufu kwa jina Diego mjini Kampala, ameshituka na kuamua kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine.
    BIN ZUBEIRY inafahamu Kiiza ana ofa tatu, moja ni klabu ya Tanzania (jina tunalihifadhi), nyingine URA na nyingine ni ya Malaysia ambako ilikuwa ende tangu mwaka jana, lakini akabanwa na Mkataba wake Yanga SC.
    Ofa ya URA na klabu ya Tanzania zina dau la usajili, lakini Malaysia anakwenda kupata mshahara mnono tu, usiopungua dola 3,000 kwa mwezi.
    URA wapo tayari kumpa Kiiza dola 40,000 za kusaini na mshahara wa dola 1,000 kwa mwezi, wakati klabu ya Tanzania bado haijafahamika imemuandalia ofa gani Mganda huyo.   
    Hayuko fiti; Ogbu Brendan Chukwudi amekuja majaribio Yanga SC, lakini kocha Brandts amesema hayuko fiti

    Yanga SC walikuwa wanataka kumpa mshahara wa dola 1,500 Kiiza na dau la usajili la dola 35,000 ambalo alikataa. Baadaye Yanga ikawa tayari kumpa Kiiza dola 40,000 lakini impe kwa awamu mbili, yeye akakataa akitaka fedha zote kwa wakari mmoja.
    Wakati ikiwa katika mazungumzo na Kiiza, Yanga ikaleta mshambuliaji kutoka Heartland ya Nigeria, Ogbu Brendan Chukwudi mwenye rekodi nzuri ya mabao ambaye hivi sasa yupo katika majaribio.
    Akimzungumzia mchezaji huyo jana, kocha wa Yanga SC, Mholanzi, Ernie Brandts alisema mshambuliaji huyo amekuja akiwa majeruhi na ambaye hana mazoezi, hivyo anampa muda kudhihirisha uwezo wake.  
    Hadi sasa, kwa uhakika haswa wachezaji wa kigeni wa Yanga SC ni watatu, ambao ni beki Mbuyu Twite, kiungo Haruna Niyonzima wote wa Rwanda na mshambuliaji Didier Kavumbangu kutoka Burundi.
    Pamoja na kumjaribu Chukwudi, Yanga SC pia ina mpango wa kuleta kiungo mshambuliaji Mbrazil, ambaye jina lake bado halijafahamika.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KIIZA AWAACHA UCHOCHORONI YANGA, APANDA KQ KUREJEA KAMPALA BAADA YA JANA KUFANYA MAZOEZI NA URA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top