• HABARI MPYA

    Wednesday, July 24, 2013

    RAIS KIKWETE AIGANDISHA STARS MWANZA, YACHELEWA KUFIKA KAMPALA

    Na Mahmoud Zubeiry, Kampala, IMEWEKWA JULAI 24, 2013 SAA 1:450 USIKU
    KIKOSI cha timu ya soka ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kimewasili salama mjini Kampala jioni ya leo tayari kwa mechi ya marudiano ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee dhidi ya wenyeji, Uganda, The Cranes Jumamosi Uwanja wa Mandela, Namboole mjini Kampala.
    Tumefuata tiketi ya CHAN; Kocha wa Stars, Kim Poulsen akiwasili Uwanja wa Ndege wa Entebe jioni ya leo

    Hata hivyo, Stars ilifika Uwanja wa Ndege wa Entebe ikiwa imechelewa tofauti na ilivyotarajiwa, kutokana na kuchelewa kuondoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza, kwa sababu ya kumpisha rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete abadilishe ndege kuelekea Bukoba, akitokea Dar es Salaam.
    Wachezaji wa Taifa Stars wakiwasili Uwanja wa Ndege wa Entebe, Uganda jioni ya leo

    Ilitarajiwa kuondoka Mwanza Saa 7.25 mchana kwa ndege ya PrecisionAir na kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe saa 8.15 mchana, lakini imechelewa kwa takriban saa mbili ili kumpisha Rais Kikwete Mwanza.
    Akiwa Uwanja wa ndege wa Mwanza, Rais Kikwete alikwenda kusalimiana na wachezaji na kuwatakia kila la heri katika mchezo wa Jumamosi.
    Mara baada ya kutua Entebe hapa, Stars ilipokewa kwa basin a kwenda Kampala mjini ambako imefikia katika hoteli ya Mt. Zion, ilikofikia pia wakati wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge Novemba mwaka jana.  
    Wachezaji wa Stars, Amri Kiemba kushoto na David Luhende kulia na kocha wa makipa, Juma Pondamali katikati wakijaza hati za Idara ya Uhamiaji Uganda ili kuingia nchini humo


    Kutoka kulia Pondamali, Kevin Yondan na Erasto Nyoni wakiwa kwenye foleni ya kwenda dirisha la Uhamiaji

    Hoi; Wachezaji wakiwa kwenye basi Uwanja wa Ndege wa Entebe, tayari kwa safari ya Kampala

    Kocha Mkuu wa Stars, Mdenmark Kim Poulsen amesema kwamba timu ilifanya mazoezi mjini Mwanza asubuhi na baada ya hapo kesho watapumzika hadi Ijumaa jioni watakapokwenda kufanya mazoezi Uwanja wa Namboole. 
    Kim amesema tangu kikosi chake kimeingia kambini Julai 14 mwaka huu, wachezaji wamekuwa wakifanya vizuri kwenye mazoezi na wako tayari kwa ajili ya mechi hiyo.
    “Uganda ni timu bora kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati. Mechi itakuwa ngumu, tunaamini tunakwenda kufanya vizuri. Tayari tunayo mikakati kwa ajili ya mechi hiyo, tunakwenda kuikamilisha Kampala,” amesema Kim.
    Juma Kaseja kulia na Simon Msuva kushoto


    Kaseja na Haroun Chanongo

    Hata hivyo, Kim amesema licha ya mwitikio mzuri wa wachezaji kwenye mazoezi lakini wanakabiliwa na changamoto ya wengi wa wachezaji kuwa wamefunga wakati wachezaji wanapokuwa kambini wanatakiwa kula, kunywa na kupumzika.
    “Hiki ni kipindi kigumu kwa mpira wa miguu, na suala la kufunga ni la kiimani ambapo hatuwezi kuwazuia wachezaji kufunga. Karibu nusu ya wachezaji wanafunga, hii ni changamoto ambayo tunaiheshimu,” amesema Kim na kuongeza kuwa ni wazi kikosi chake cha kwanza kitakuwa na mabadiliko baada ya beki Shomari Kapombe kwenda kwenye majaribio nchini Uholanzi.
    Kikosi cha Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kilichotua hapa ni makipa Juma Kaseja, Mwadini Ali na Ali Mustafa. Mabeki ni Aggrey Morris, David Luhende, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Nadir Haroub na Vincent Barnabas.
    Watoto wa magwiji; Watoto wa magwiji wa zamani wa soka nchini, Mrisho Ngassa ambaye baba yake Khalfan Ngassa aling'ara Pamba ya Mwanza na Simba SC na Salum Abubakar kushoto, ambaye baba yake, Abubakar Salum Sure Boy aling'ara SIgara na Yanga SC wakiwa Entebe

    Viungo ni Amri Kiemba, Athuman Idd, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Khamis Mcha, Mudhathir Yahya, Salum Abubakar na Simon Msuva. Washambuliaji ni John Boko, Juma Luizio na Mrisho Ngasa.
    Baada ya kufungwa 1-0 katika mchezo wa kwanza wiki iliyopita mjini Dar es Salaam, Stars sasa inatakiwa kushinda 2-0 ili kukata tiketi ya kwenda Afrika Kusini mwakani, zitakapopigwa Fainali za CHAN, au ishinde 1-0 na mchezo uamuliwe kwa mikwaju ya penalti.
    John Bocco kulia na kocha Msaidizi, Syvlester Marsh
    Ikiwa kambini mjini Mwanza, Stars pia imekuwa ikifanya mazoezi ya kupiga penalti, kujiweka tayari kwa zoezi hilo endapo litatokea.
    The Cranes imeendelea na mazoezi jioni ya leo Uwanja wa Namboole na kocha wake, Mserbia Milutin Sredojevic ‘Micho’ amesema kwamba kikosi chake kipo tayari kukamilisha kazi kilichoianza Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: RAIS KIKWETE AIGANDISHA STARS MWANZA, YACHELEWA KUFIKA KAMPALA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top