• HABARI MPYA

  Jumatano, Julai 31, 2013

  MAKOSA HAYA WAYAFANYIE STARS TU, KWENYE KLABU ZAO…

  IMEWEKWA JULAI 31, 2013 SAA 1:08 ASUBUHI
  MPIRA wa miguu ni mchezo wa makosa, hilo ni neno maarufu katika familia ya kandanda, lakini si wote wanaokubaliana na kauli hii.
  Kwa kiasi kikubwa ndani ya soka yetu Tanzania, mchezaji anapokosea hachukuliwi kama ni hali ya kimchezo na watu huzama ndani na kuibua mitazamo tofauti, kubwa mchezaji kahujumu timu.
  Moja kati ya sababu ambazo Simba SC walikuwa wanazitaja kuwafanya waachane na kipa na Nahodha wao wa siku nyingi, Juma Kaseja ni bao la kwanza alilofungwa katika mechi dhidi ya watani, Yanga SC ambao walishinda 2-0 Mei mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

  Katika mchezo huo wa kufunga pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mpira wa kona ulimpita Kaseja ukaenda kumkuta Didier Kavumbangu akafunga. Sasa Simba SC, wanasema ule mpira ulimpita mbele yake Kaseja, hivyo hakustahili kutoudaka hadi ukamkuta Mrundi, Kavumbangu akafunga.
  Wanapunguza makali kwa kusema ulimpita kwa sababu uwezo umepungua, lakini wanaamini alipewa hongo afungishe. Ni kweli, Kaseja alifungwa bao rahisi la kwanza, lakini makipa wengi tu bora duniani nao pia hufanya makosa si Kaseja peke yake.
  Lakini yote mazuri aliyoyafanya miaka yote, yalisahaulika ndani ya dakika 90 na akaonyeshwa mlango wa kutokea Msimbazi. Ukweli ni kwamba, lazima timu zetu zibadilike na zielewe soka ni mchezo wa makosa na ndiyo yanasababisha matokeo. Kama wapinzani hawakosei, mabao yatapatikanaje?
  Neno moja kubwa huzungumzwa baada ya mchezo, iwe na makocha au wachambuzi kweli na wasio uchwara, nafasi. Timu kutengeneza nafasi na kutumia ni kipaumbele cha ushindi na timu kufanya kosa la kuwapa wapinzani nafasi za kufunga ni pigo.
  Kwa mfano ukirejea mchezo wa kuwania tiketi ya kucheza michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, Jumamosi Uwanja wa Mandela, Namboole mjini Kampala, ambao wenyeji Uganda waliifunga Tanzania 3-1, ni makosa ya wachezaji wetu yaliyowapa The Cranes tiketi ya Afrika Kusini mwakani.
  Kipindi cha kwanza kilimalizika timu hizo zimefunga 1-1 na timu yoyote ambayo ingeongeza bao ingefuzu CHAN, kwani katika mchezo wa kwanza Uganda walishinda pia 1-0 Dar es Salaam. Stars ingeshinda 2-1 ingefuzu kwa faida ya mabao ya ugenini na ilijipanga kwa ajili hiyo kipindi cha pili.
  Wakati dakika 45 za kwanza zinamalizika, mashabiki wa Uganda walikuwa kama wamemwagiwa maji Uwanja wa Namboole, wakiamini wakati mchezo ukiwa 1-1, lolote lingeweza kutokea.
  Lakini kosa moja tu la beki David Luhende kuunawa mpira kwenye eneo la hatari, liliwapa penalti wenyeji na Brian Majwega akaenda kumtungua vizuri Juma Kaseja dakika ya 48. Ni ajabu kweli kweli, Luhende aliunawa mpira akiwa yuko peke yake kwenye boksi. Alikuwa anaweza kuuondosha mpira kwenye eneo la hatari. Alikuwa anaweza kubutua mbele au kutoa pasi, kwa sababu hakuwa amezongwa.
  Lakini akafanya madaha mwishowe mpira ukapanda mkononi na refa alikuwa makini mno kuona makosa yanayofanywa na wachezaji wa Stars, likatengwa tuta, tukafungwa bao la pili.  
  Stars ilizinduka tena na kuanza kushambulia lango la Uganda, ingawa na wenyeji nao waliendelea kushambulia.  
  Hata hivyo, kosa lingine la Salum Abubakar ‘Sure Boy’ katika dakika ya 62 liliipa Uganda bao la tatu. Stars walipata kona, ilipopigwa ikaokolewa na mpira ukamkuta Sure, lakini wakati Simon Msuva na Ngassa wamefungua pembeni, kiungo huyo akataka kupiga chenga katikati ya watu wawili.
  Akapokonywa mpira ikapigwa pasi ndefu kwa Hassan Waswa wakati huo wachezaji wote wa Stars wamepanda kwa ajili ya kona, Brian Majwega akafungua kushoto. Waswa akamvuta beki pekee wa Stars aliyekuwa amebaki nyuma, Kevin Yondan akapeleka pasi kwa Majwega, akatia krosi Kalanda akamtungua Kaseja.
  Ilikuwa timu ya taifa, makocha na viongozi wa Kamati ya ushindi pamoja na TFF wanajua soka ni mchezo wa makosa na kambi ijayo bila shaka wote Sure na Luhende wataitwa na ni imani kwamba wamepata fundisho kubwa kutokana na makosa yao, yaliyoigharimu timu.
  Ila kama makosa haya Sure angefanya Azam, tena dhidi ya moja ya timu mbili, Simba au Yanga, ingekuwa habari nyingine. Endapo Luhende angefanya kosa kama lile akiwa na jezi Yanga, tena ikicheza na Simba au Azam, leo hadithi ingekuwa tofaiti. Kwanza, kwa Yanga angetokea mlango gani?
  Kweli hii si sahihi, mashabiki wa soka nchini hususan wa Simba na Yanga na viongozi wao kwa ujumla, lazima ufike wakati wabadilike na waipe heshima yake soka. Mpira ni mchezo wa makosa. Alamsiki. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: MAKOSA HAYA WAYAFANYIE STARS TU, KWENYE KLABU ZAO… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top