• HABARI MPYA

  Jumapili, Julai 21, 2013

  BANGI ZINATUHARIBIA SANA WACHEZAJI WETU, WENGI BONGO ZAO ZIMEOZA BADO WADOGO

  IMEWEKWA JULAI 21, 2013 SAA 1:30 ASUBUHI
  TUNAZUNGUMZA sana kwenye vikao vyetu kuhusu wachezaji ambao tunaona kabisa wanaathirika kwa utumiaji wa dawa za kulevya.  Hata baadhi ya mashabiki wamekwishagundua wachezaji fulani fulani, viwango vyao vinaathirika kwa utumiaji wa dawa za kulevya.
  Taratibu idadi ya watumiaji mihadarati katika soka yetu inaongezeka na sasa vizazi na vizazi vinarithi desturi hii.
  Mwaka juzi, baada ya kushuka kwa kasi kwa kiwango cha soka Afrika Kusini kulilishitua mno Shirikisho la Soka nchini humo na hatua mbalimbali zikachukuliwa kuhakikisha mambo yanakaa vizuri tena.

  Afrika Kusini wanataka kurejesha makali yao kwenye soka ya Afrika. Wamegundua makosa yao; sasa wachezaji wa kigeni hawana nafasi ya kutawala katika Ligi ya Afrika Kusini.
  Limewekwa azimio maalumu kwa kuhakikisha klabu kubwa nchini humo kama Kaizer Chiefs, Orlando Pirates, SuperSport United, Jomo Cosmos, Santos na nyingine zinakuwa mstari wa mbele katika kuinua vipaji vya wachezaji wa nyumbani.
  Wenzetu wameamua, na kweli wamefanya, ndiyo maana utaona wachezaji walionunuliwa miaka ya karibuni na klabu kubwa za huko kwa mfano kipa Dennis Onyango Julai 8, mwaka huu alitemwa SuperSport United na kwa bahati nzuri akasajiliwa na katimu kadogo tu; Mpumalanga Black Aces.
  Brian Umuny wa Uganda pia naye alitemwa na timu hiyo akaenda University of Pretoria FC kabla ya kuja Azam na ni wakati huo huo gazeti la New Vision liliandika kwamba, Arsenal ilikuwa inamtaka mchezaji huyo na kumuhitaji kwa majaribio baada ya kuvutiwa na rekodi yake ya ufungaji wa mabao.
  Hakuwa mchezaji wa kuachwa kwenye timu inayojiendesha kibiashara na kisasa kama SuperSport United, lakini kwa sababu sera imepitishwa, wameiheshimu.
  Kwetu idadi ya wachezaji wa kigeni ilipunguzwa kwa sababu wengi hawakuwa na viwango- haikuwa sababu inawanyima nafasi wachezaji wa nyumbani. Tatizo letu ni ushabiki, tunataka klabu zetu ziwe imara bila kuzingatia maslahi ya soka yetu.
  Hiyo ni hatua moja wenzetu wamechukua, lakini katika kutafuta suluhisho la kuzama kwa soka yao, wameamua kupiga marufuku na bangi kwenye soka yao.
  Vipimo vinatembea na akibainika mchezaji anavuta bangi, amejifuta kwenye familia ya soka nchini humo. Ni hatua ya kupongeza kweli, sasa soka ya Afrika Kusini ipo kwenye kikombe cha matumaini mapya.
  Vipi kwetu Tanzania? Tunafahamu fika kuna wachezaji wetu wamepigika kisoka kwa sababu ya utumiaji wa dawa za kulevya. Walianza kuvuta bangi, wakawa wavutaji kupindukia na sasa wanajidunga sindano za dawa za kulevya. Wamechoka.
  Tena wale wale ambao miaka mitatu iliyopita tulikuwa tunawatabiria kucheza Ulaya, lakini sasa hali imebadilika na tunachowatabiria kwa sasa ni kutemwa wakati wowote kwenye klabu zao kadiri michango yao inavyozidi kupungua.
  Wavuta bangi kwenye soka yetu, hao ni wengi sana na wengine wapo timu ya taifa pale. Tunawekeza nini kwenye soka yetu? Umefika wakati sasa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likachukua hatua za kupambana na hali hii. 
  Hii inapaswa kuingizwa kwenye kanuni na utaratibu wa kuwapima wachezaji wetu ukaanza mara moja. Tuweke kando ushabiki na tuwahukumu wachezaji bila kuwaangalia huyu ni wa klabu gani.
  Kwani bila hivyo, na hawa wanaoibuliwa kwenye Copa Coca Cola nao watatumbukia tu kwenye janga hilo, iwapo hakutakuwa na tishio la kuwaogopesha kujitumbukiza kwenye utumiaji wa dawa za kulevya.
  TFF iweke kanuni za adhabu, tena kali dhidi ya wachezaji watumiao dawa za kulevya nchini. Hii itakuwa njia nzuri ya kuwaengua wachezaji sumu kwenye soka yetu na kuondoa uwezekano wa kuambukiza wengine tabia hii.
  Tunahitaji kujifunga mkanda na kupambana haswa kuhakikisha soka yetu inaimarika kwa kupigana katika kila nyanja, ili mambo yawe sawa. Tuanze kwa hili la dawa za kulevya, hususan bangi. Sidhani kama ipo timu ya Ligi Kuu ambayo inakosa wachezaji wasiopungua watatu wanaovuta bangi. Sidhani. Kwa kweli bangi zinaharibu sana wachezaji wetu na wengi wao bongo zao zimeoza bado wadogo tu. Ramadhan kareem. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: BANGI ZINATUHARIBIA SANA WACHEZAJI WETU, WENGI BONGO ZAO ZIMEOZA BADO WADOGO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top