• HABARI MPYA

  Jumamosi, Julai 27, 2013

  STARS YAKUNG'UTWA 3-1 NA UGANDA, NJE CHAN

  Na Mahmoud Zubeiry, Kampala, IMEWEKWA JULAI 27, 2013 SAA 12:00 JIONI
  NDOTO za Tanzania kucheza Fainali za pili za michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, zimezimika leo baada ya kufungwa na Uganda mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa.
  Kwa matokeo hayo, Tanzania inayofundishwa na kocha Mdenmark, Kim Poulsen imetolewa kwa jumla ya mabao 4-1, baada ya wiki mbili zilizopita kufungwa 1-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Shujaa wa The Cranes, au Korongo wa Kampala inayofundishwa na Mserbia, Milutin Sredojevic ‘Micho’ leo alikuwa ni Frank Kalanda anayechezea Timu ya Mamlaka ya Mapato (URA) ya hapa aliyefunga mabao mawili. 
  Wababe wetu; Uganda wakishangilia bao lao la tatu leo

  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Kanoso Abdoul Ohabee, aliyesaidiwa na Andirvoavonjy Pierre Jean Eric na Jinoro Velomanana Ferdinand wote kutoka Madagascar, hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1.
  Uganda walianza mchezo kwa kasi ndani ya dakika 10 za mwanzo walilitia sana misukosuko lango la Stars na hatimaye wakafanikiwa kupata bao dakika ya saba, mfungaji Frank Kalanda, baada ya kutokea kizazaa langoni mwa Stars.
  Marikiti; Kipa wa Tanzania, Juma Kaseja akiruka upande wa pili wa mkwaju wa penalti wa Brian Majwega

  Hata hivyo, baada ya bao hilo, mabeki wa Stars walilaumiana kidogo na kipa wao kwa kosa lililoruhusu bao, lakini wakazinduka na kuanza kucheza vizuri.
  Stars ilianza kushambulia kwa kutumia mipira mirefu ya pembeni iliyokuwa ikipelekwa kwa Mrisho Ngassa na kwa mtindo huo, ilifanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika ya 14.
  Ngassa alipokea mpira mrefu wa Athumani Iddi ‘Chuji’ upande wa kushoto mwa Uwanja, akamtoka beki wa Uganda Nicolas Wadada na kutia krosi maridadi iliyowapita mabeki wa kati wa Cranes na kumkuta Amri Kiemba aliyefumua shuti zuri mpira ukatinga nyavuni.
  Baada ya bao hilo, Uganda walipoteana na Stars ikaanza kutawala mchezo, ingqawa haikufanikiwa kupata bao. Dakika ya 43, Stars ilipata pigo baada ya kiungo wake, Frank Domayo kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Simon Msuva.
  Mfungaji wetu; Mfungaji wa bao la Stars, Amri Kiemba akiwatoka wachezaji wa Uganda

  Kipindi cha pili Stars walikianza vizuri, dakika mbili za mwanzo, lakini kosa moja tu la beki David Luhende kuunawa mpira kwenye eneo la hatari, liliwapa penalti wenyeji na Brian Majweda akaenda kumtungua vizuri Juma Kaseja dakika ya 48.
  Stars ilizinduka tena na kuanza kushambulia lango la Uganda, ingawa na wenyeji nao waliendelea kushambulia.  
  Hata hivyo, kosa la Salum Abubakar 'Sure Boy' katika dakika ya 62 liliipa Uganda bao la tatu. Stars walipata kona, ilipopigwa ikaokolewa na mpira ukamkuta Sure Boy, lakini wakati Simon Msuva na Ngassa wamefungua pembeni, kiungo huyo akataka kupiga chenga katikati ya watu wawili.
  Akapokonywa mpira na Hassan Waswa wakati huo wachezaji wote wa Stars wamepanda kwa ajili ya kona, Brian Majwega akafungua kushoto. Waswa akamvuta beki pekee wa Stars aliyekuwa amebaki nyuma, Kevin Yondan akapeleka pasi kwa Majwega, akatia krosi Kalanda akamtungua Kaseja.
  Mchezo ulikuwa wa Uganda tangu hapo, Stars wakicheza kwa presha ya kutoruhusu mabao zaidi na wakati huo huo wakisaka mabao, jambo ambalo liliwapa kazi nyepesi wenyeji kuutawala mchezo.
  Kikosi cha Stars kilikuwa; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, David Luhende/Vincent Barnabas dk78, Aggrey Morris, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo/Simon Msuva dk43, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco ‘Adebayor’/Haroun Chanongo dk78, Amri Kiemba na Mrisho Ngassa.
  The Cranes; Hassan Muwonge, Hassan Waswa, Nicolas Wadada, Habib Kavuma, Savio Kabugo, Richard Kasaga, Dennis Iguma, Said Kyeyune/Ntege Ivan dk62, Joseph Mpande/Simon Okwi dk 72, Frank Kalanda/Lawrence Nduga dk 89 na Brian Majwega. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: STARS YAKUNG'UTWA 3-1 NA UGANDA, NJE CHAN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top