• HABARI MPYA

    Wednesday, July 24, 2013

    USHAURI WA BURE KWA YANGA SC KUHUSU BRENDAN OGBU CHUKWUDI

    IMEWEKWA JULAI 24, 2013 SAA 12:00 ASUBUHI
    HAKUNA shaka- Mnigeria aliye katika majaribio Yanga SC, Brendan Ogbu Chukwudi ni mchezaji mzuri na hiyo ni kutokana na rekodi na wasifu wake.
    Shaka ni juu ya maumivu yanayomuandama tangu awasili Dar es Salaam wiki iliyopita kwa mazoezi- je ni ya muda mfupi, au mrefu.
    Chukwudi, ilikuwa aanze katika mechi ya Jumapili ya kirafiki dhidi ya URA ya Uganda, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, lakini akaumia wakati wa kupasha misuli moto na kuondolewa katika mchezo huo ulioisha kwa sare ya 2-2.
    “Inasikitisha, nimeumia tena. Safari hii ni kifuniko cha goti. Sijui ni nini hapa, ila hakuna namna nyingine zaidi ya kupumzika na kupata tiba kwa sasa,“alisema Chukwudi Jumapili akiwa anatazama mechi hiyo.

    Wakati nazungumza naye, nilikuwa namtazama usoni- sura yake inawakilisha masikitiko na maumivu ya moyo juu ya hali inayomkabili kwa sasa. Inamuumiza. Alikuja majaribio kwa sababu alijiamini anaweza na yuko sawa. Lakini bahati mbaya imemkuta na kocha wa Yanga SC, Mholanzi Ernie Brandts amesema anampa muda Mnigeria huyo apone na kuonyesha uwezo wake mazoezini, ilia atoe baraka zake kwa uongozi asajiliwe.
    Daktari wa Yanga SC, Nassor Matuzya amesema inaonekana mchezaji huyo ana matatizo mengi na ambayo ni ya muda mrefu kwake. “Kwanza ilikuwa ni kifundo cha mguu. Tumehangaika naye na akawa anacheza, sasa hivi tena linaibuka la kufuniko cha goti. Kwa kweli hii hali inatusikitisha na hatujui la kufanya kwa sasa,”alisema.
    Lakini Dk Matuzya pia akaushauri uongzi wa Yanga SC kwamba kaunzia sasa uweke utaratibu wa kuwapima afya wachezaji kabla ya kuwaleta kwenye timu, ili kuepuka gharama zisizo za lazima.
    Kinachoonekana ni kama benchi la Ufundi la Yanga SC halijaridhishwa na mchezaji huyo na wanahofia tu kuwaambia ukweli viongozi hadi watakapojionea wenyewe.
    Akijua kabisa mchezaji huyo ni majeruhi na hayuko fiti- lakini kocha Brandts jana alitaka kumpanga Chukwudi kama si kuumia wakati anapasha misuli moto.
    Kulingana na wasifu wake na rekodi zake- Chukwudi aliyetokea Heartland FC ya Nigeria, ni mchezaji mzuri na hadi msimu uliopita alikuwa moto katika Ligi Kuu ya Nigeria kiasi hadi cha kuitwa timu ya taifa ya nchi hiyo, Super Eagles.    
    Mchezaji huyo wa zamani wa Enugu Rangers ya Nigeria sasa mustakabali wake ni tata Yanga SC- haijulikani kama uongozi utacheza kamari kwa kuamua kumsajili na kumtibu au kuachana naye na kutafuta mchezaji mwingine.
    Narudia, hakuna shaka Chukwudi ni mchezaji mzuri- lakini suala la maumivu yake ni ambalo Yanga SC wanatakiwa kulifanyia kazi kwa sasa. Yanga wanaweza kuamua kuachana naye na kumbe si maumivu ya muda mrefu, na wakapoteza mchezaji mzuri. Na wanaweza kumsajili kumbe ana maumivu sugu, wakaingia hasara.
    Rahisi tu, Yanga wampeleke mchezaji huyo kufanyiwa vipimo ili ijulikane ukubwa wa maumivu yake na baada ya hapo, majibu yatawafanya waamue kuwa naye au kuachana naye. 
    Wanachotafuta Yanga SC ni mshambuliaji atakayewasaidia katika Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kwenye ligi yetu hapa, akina Jerry Tegete na Didier Kavumbangu wanatosha sana na wanaweza- na ni hao hao waliipa ubingwa timu hiyo msimu uliopita.
    Chukwudi anasema kabla ya kuja Yanga, alikuwa Misri ambako aliitwa na klabu moja iliyotaka kumsajili, lakini kutokana na vurugu za kisiasa zinazoendelea nchini humo sasa akaamua kuondoka kuja Tanzania kufuata wito wa Yanga SC.
    Na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga SC, Abdallah Bin Kleb alisema walimfuatilia kwa muda mrefu na hadi kumleta nchini wameridhika naye ni bora.
    “Huyu ni bora, anajua kufunga, ni kijana mdogo na uwezo mkubwa sana. Aliitwa timu ya taifa ya Nigeria, kitu ambacho kwa nchi kama ile yenye wachezaji wengi wazuri kinaashiria huyu ni mchezaji mzuri sana,”alisema.
    Naungana na Kleb, kuitwa timu ya taifa ya Nigeria si jambo rahisi kwa sababu ukweli ni kwamba nchi ile ina wachezaji wengi wazuri. Lazima Chukwudi alifanya vitu akaonekana. 
    Nchini Nigeria, vyombo vya habari vinamsifu Brendan kama mshambuliaji kinda mwenye nguvu, kasi, uwezo wa hali ya juu na ufundi pia. Klabu ya Esperance Sportif ya Tunisia ilijaribu kumsajili msimu huu kujiongezea nguvu katika kampeni zake za kuwania taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini pande hizo mbili zikashindwa kufikia makualiano.
    Ni hatari mno anapoingia kwenye eneo la hatari na ana kipaji cha hali ya juu cha kufunga kwa kichwa na miguu yote- na ni mmaliziaji mzuri.
    Mshambuliaji huyo alijiunga na Heartland msimu uliopita akitokea Enugu Rangers, aliyoanza kuichezea mwaka 2008. Kisoka Ogbu aliibukia Unth Enugu, kabla hajajiunga na Enugu Rangers.
    Brendan aliifungia mabao 11 Enugu Rangers na kuwa mfungaji bora wa klabu katika Ligi Kuu  msimu wa 2010/2011 na akaihama klabu hiyo, akiwa ameifungia jumla ya mabao 30 kwenye mashindano yote.
    Alikuwa miongoni mwa wachezaji wapya walioitwa na kocha Stephen Keshi katika kikosi cha Nigeria, kiliochokwenda kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Afrika Kusini pamoja na Tony Okpotu wa Lobi Stars, Mannir Ubale wa Kano Pillars na Fidelis Saviour, aliyekuwa FC Taraba kabla ya kuhamia Enyimba. 
    Keshi alijumuisha wachezaji 15 wanaocheza Ulaya katika kikosi hicho, akiwemo kiungo wa Chelsea, John Mikel Obi kwa ajili ya mchezo dhidi ya Liberia mjini Calabar, Oktoba 13, mwaka jana.
    Kikosi hicho kilikuwa; Makipa: Chigozie Agbim (Warri Wolves) na Daniel Akpeyi (Heartland). Mabeki: AzubuikeEgwuekwe (Warri Wolves), Papa Idris (Kano Pillars), Godfrey Oboabona (SunshineStars), Umar Zango (Kano Pillars), Solomon Kwambe (Sunshine Stars), BasseyEzekiel (Lobi Stars) na Kingsley Udoh (Heartland)
    Viungo: EjikeUzoenyi (Enugu Rangers), Sunday Mba (Warri Wolves), Gabriel Reuben (KanoPillars), Henry Uche (Enyimba), Christian Ofili (ABS), Solomon Jabason (AkwaUnited), Philip Asuquo (3SC) na Gomo Onduku (Sharks).
    Washambuliaji: FidelisSaviour (FC Taraba), Sanusi Sani (Gombe United), Izu Azuka (Sunshine Stars), Brendan Ogbu (Heartland), Tony Okpotu (Lobi Stars) na Mannir Ubale (Kano Pillars).
    Huyu ni mchezaji mzuri na Yanga SC hawatakiwi kuwa na papara juu yake- kumsubiri hata kwa miezi mitatu si mbaya, iwapo vipimo vya kitaalamu vitaonyesha maumivu yake si ya kutisha. Ushauri wa bure kwa viongozi wa Yanga, wakamfanyie vipimo mchezaji huyo ili kujua ukubwa wa maumivu yake na baada ya hapo waamue, kusuka au kunyoa. Ramadhani kareem. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: USHAURI WA BURE KWA YANGA SC KUHUSU BRENDAN OGBU CHUKWUDI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top