• HABARI MPYA

  Jumatano, Julai 31, 2013

  YANGA SC WATIMULIWA LOYOLA, WAHAMIA KIJITO

  Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JULAI 31, 2013 SAA 1:35 ASUBUHI
  UONGOZI wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam umeizuia klabu ya Yanga SC kufanya mazoezi kwenye Uwanja wake, ili kupisha maandalizi ya sherehe maalum za shule hiyo wiki hii.
  Sasa Yanga wanahamia kwenye Uwanja mbovu zaidi wa Kijinyonama hadi Ijumaa sherehe za Loyola zitakapomalizika, ndipo watarejea kwenye Uwanja mzuri kidogo kwa mazoezi.
  “Yanga hawapo hapa, kuna sherehe za shule na tumewasimamisha kwa muda kuutumia uwanja wetu hadi Ijumaa, wamehamia Kijitonyama,”alisema mlinzi mmoja wa Loyola alipoulizwa na BIN ZUBEIRY leo.
  Kikosi cha Yanga SC

  Wakati maandalizi ya Yanga yakielekea kuendelea kusuasua, wapinzani wao katika mchezo wa kufungua pazia la Ligi Kuu, Azam FC wanatarajiwa kuondoka nchini mchana wa Jumamosi kwenda Johanesburg, Afrika Kusini kuweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na mchezo huo pamoja na msimu mpya kwa ujumla.
  Kwa takriban mwezi wote huu, Azam imekuwa ikijifua katika Uwanja mzuri wa nyasi bandia, Azam Complex, Chamazi pamoja na kufanya mazoezi ya ufukweni na gym na nchini Afrika Kusini pamoja na kwenda kuweka kambi ya mazoezi, pia itacheza mechi nne za kujipima nguvu dhidi ya timu kubwa za huko.
  Ingawa bado ratiba ya mechi za Azam nchini humo haijajulikana, lakini inafahamika miongoni mwa timu zitakazocheza na Azam ni Orlando Pirates, Supersport United, Kaizer Chiefs na Mamelodi Sundowns.
  Kuna uwezekano Azam ikacheza mechi zaidi kulingana na namna ambavyo timu zaidi nchini humo zitavuwi kucheza nayo.
  Azam inatarajiwa kurejea nchini siku moja kabla ya kucheza mechi ya kuwania Ngao ya Jamii kuashiria kufungua pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Yanga SC, Agosti 17, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Safari hii Azam, washindi wa pili mara mbili mfululizo wa Ligi Kuu wamepania kutwaa Ngao mbele ya Yanga, baada ya mwaka jana kufungwa na Simba SC na kocha Muingereza Stewart Hall anajiandaa kikamilifu kwa ajili hiyo.    
  Yanga SC bado haijajulikana lini angalau itaingia kambini kujiandaa na mchezo huo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: YANGA SC WATIMULIWA LOYOLA, WAHAMIA KIJITO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top