• HABARI MPYA

    Monday, January 07, 2019

    TFF YAMREJESHA KEVELA KUGOMBEA UMAKAMU MWENYEKITI YANGA SC

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Rufaa ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemrejesha Yono Kevela kuendelea kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga katika uchaguzi wa Januari 13, mwaka huu mjini Dar es Salaam.
    Hiyo ni baada ya Kevela kukata rufaa akilalamikia maamuzi ya kuenguliwa jina lake kwenye majina ya wagombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti, kwa madai aliomba nafasi mbili, nyingine ya Uenyekiti.
    Na baada ya kikao cha Kamati hiyo ilikutana chini ya Mwenyekiti wake Kenneth Mwenda kusikiliza utetezi wa Kevela dhidi ya Kamati ya Uchaguzi iliamua kumrudisha kuwa mmoja wa Wagombea katika nafasi hiyo.



    Yono Kevela (kulia) amerejeshwa kuendelea kugombea Umakamu Mwenyekiti Yanga katika uchaguzi wa Januari 13

    Rufaa nyingine iliyowasilishwa katika Kamati hiyo ni ya Mhandisi Leonard Marango ambaye hakuridhishwa na maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi kama Kevela.
    Kamati ilisikiliza utetezi wa Marango aliyesema kwamba hakufika kwenye usaili katika siku zillizopangwa kwa sababu alisafiri na kuchelewa kufika kwa wakati.
    Lakini baada ya kusikiliza utetezi wake, Kamati ilijiridhisha kuwa Marango alishindwa kuhudhuria usaili bila taarifa yoyote hivyo imetupilia mbali rufaa hiyo.
    Kevela sasa anaungana na Titus Eliakim Osoro na Salum Magege Chota kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti, wakati wagombea Uenyekiti ni Dk. Jonas Benedict Tiboroha, Mbaraka Hussein Igangula na Erick Ninga.
    Kuna wagombea 16 wa nafasi za Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu ambao= ni Hamad Ally Islam, Benjamin Jackson Mwakasonda, Sylvestre Haule, Salim Seif, Shafil Amri, Said Kambi, Dominick Francis, Seko Jihadhari, Ally Omar Msigwa, Arafat Ally Hajji, Frank Kalokola, Ramadhani Said, Leonard Marango, Bernard Faustin Mabula, Christopher Kashiririka na Athanas Peter Kazige.
    Uchaguzi wa Januari 13 mjini Dar es Salaam ni maalum kuziba nafasi za wagombea waliojiuzulu kwa wakati tofauti baada ya uchaguzi wa Juni 11 mwaka 2016.
    Waliojiuzulu ni aliyekuwa Mwenyekiti Yussuf Manji, Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na Wajumbe wanne, Omary Said Amir, Salum Mkemi, Ayoub Nyenzi na Hashim Abdallah.
    Waliobaki katika Kamati ya Utendaji ni wane tu ambao ni Siza Augustino Lymo, Tobias Lingalangala, Samuel Lukumay na Hussein Nyika.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YAMREJESHA KEVELA KUGOMBEA UMAKAMU MWENYEKITI YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top