• HABARI MPYA

    Sunday, July 08, 2018

    KILIMANJARO QUEENS KUANZA NA RWANDA CHALLENGE YA WANAWAKE RWANDA JULAI 19

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM 
    MABINGWA watetezi wa mashindano ya Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Queens itaanza kampeni ya kutetea ubingwa wa michuano hiyo kwa kuwavaa wenyeji Rwanda (She-Amavubi) katika mechi ya ufunguzi itakayofanyika Julai 19 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nyamirambo.
    Michuano hiyo inayoandaliwa na Baraza la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) mwaka huu itashirikisha timu tano na itachezwa kwa mtindo wa ligi.
    Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye alisema wenyeji Rwanda wako tayari kwa kusimamia michuano hiyo na kuongeza kuwa kabla ya mechi hiyo ya ufunguzi, kutakuwa na mchezo kati ya Kenya dhidi ya Uganda.

    Musonye alisema kuwa Kilimanjaro Queens itashuka tena dimbani saa 8:00 mchana Julai 21 mwaka huu kuikabili Kenya wakati siku hiyo kuanzia saa 10:00 jioni Ethiopia wataivaa Uganda, mechi zote zikichezwa kwenye Uwanja wa Nyamirambo.
    Alisema kuwa mabingwa hao watetezi watacheza mechi yao ya tatu dhidi ya Uganda Julai 23 huku itamaliza mchezo wake wa mwisho kwa kupambana na Ethiopia ifikapo Julai 27.
    "Bado sijafurahishwa na uamuzi ambao umefanywa na baadhi ya vyama, haijawapa kipaumbele wanawake kutumia nafasi hii kuonyesha vipaji vyao, tuna nchi wanachama 12, na michuano hii inashirikisha timu tano, si haki kwa mabinti zetu," alisema Musonye.
    Aliongeza kuwa imefika wakati nchi zikaweka pembeni tofauti zao za kisiasa na kuruhusu vijana kushiriki kila mashindano yanayoandaliwa na kuwaimarisha na baadaye kupambana kwenye mechi za michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
    Aliongeza kuwa kutokana na idadi chache ya timu zitakazoshiriki michuano hiyo, wamepanga mashindano hayo yafanyike kwa mtindo wa ligi na timu itakayokuwa na pointi nyingi itatangazwa kuwa bingwa mpya.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KILIMANJARO QUEENS KUANZA NA RWANDA CHALLENGE YA WANAWAKE RWANDA JULAI 19 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top