• HABARI MPYA

    Friday, September 22, 2023

    WIZARA ZA MICHEZO TANZANIA, KENYA NA UGANDA ZAJADILI MAANDALIZI AFCON 2027


    TIMU ya Wataalamu wakiongozwa na Makatibu Wakuu wa michezo kutoka Tanzania, Kenya na Uganda ambazo kwa pamoja zinaomba kuwa wenyeji wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) kupitia maombi ya EA Pamoja Bid imekutana kujadili maandalizi.
    Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho kilichofanyika Septemba 21, 2023 jijini Dar es Salaam kufuatia barua Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ambalo limeainisha na kuitaja Septemba 27, 2023 ndiyo siku ya kupiga kura Cairo, Misri kuamua ni nchi gani itapewa dhamana ya kuandaa michuano hiyo 2027.
    “Tuliona ni muhimu kama nchi zetu ambazo tunaomba kwa pamoja tukutane tupange mikakati ya namna ya kupata ushindi, leo tulikuwa na Makatibu Wakuu wa Michezo kutoka Tanzania, Kenya na Uganda na kujadili kwa kina ili tufanikiwe na ni kikao cha kujipanga kwa ajili ya Mawaziri ambao watakutana hapa kesho Septemba 22, 2023 kwa ajili ya kupanga mikakati hiyo” amesema Katibu Mkuu Bw. Yakubu.
    Katibu Mkuu, Yakubu amesema kuwa CAF wanaangalia ni miundombinu ambayo ipo tayari na mipango ya miundombinu inayojengwa.
    Ameongeza kuwa maombi hayo yanaungwa mkono na Marais wan chi zote tatu Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda na William Ruto wa Kenya wote kwa pamoja wanaunga mkono na wamepokea vitabu vya maombi hayo na wametoa maelekezo kazi hiyo iendelee.
    Viongozi waliohudhuria kikao hicho ni Mhandisi Peter Kitum, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Vijana, Sanaa na Michezo, Ambros Tashobya, Mwakilishi wa Katibu wa Wizara ya Michezo Uganda ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Uganda, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa Leodigar Tenga, Katibu Mtendaji Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha pamoja na maafisa kutoka Kenya, Uganda na wenyeji Tanzania pamoja na viongozi wa Mashirikisho ya Mpira wa Miguu kuitoka Kenya na Uganda.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WIZARA ZA MICHEZO TANZANIA, KENYA NA UGANDA ZAJADILI MAANDALIZI AFCON 2027 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top