• HABARI MPYA

    Thursday, June 04, 2020

    AZAM FC KUJIPIMA KWA TRANSIT CAMP JUMAMOSI KABLA YA KUIVAA MBAO FC JUNI 14 CHAMAZI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KATIKA kujiandaa na mchezo wake wa kiporo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Mbao FC ya Mwanza Juni 14, mwaka huu Azam FC watakuwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Transit Camp Jumamosi.
    Afisa Habari wa Azam FC, Thabit Zakaria amesema kwamba mechi zote mbili zitafanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Darves Salaam na zitaanza Saa 1:00 usiku.
    Wiki iliyopita Bodi ya Ligi ilitoa ratiba ya mechi za viporo za Ligi na mbali na Azam kumenyana na Mbao FC, mabingwa watetezi, Simba SC watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting Juni 14 pia Uwanja wa Taifa.
    Awali, Juni 13 Mwadui FC watakuwa wenyeji wa Yanga SC Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga wakati Coastal Union wataikaribisha Namungo FC Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
    Vigogo Yanga SC watahitmisha duru la mechi za viporo kwa kumenyana na JKT Tanzania Juni 17 Uwanja wa Taifa kabla Ligi Kuu kuanza tena rasmi Juni 20 na kufikia tamati Julai 26 kufuatia kusimama tangu Machi 17 kwa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutokana na mlipuko wa maambukizi ya virusi vya corona.  
    Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
    Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC KUJIPIMA KWA TRANSIT CAMP JUMAMOSI KABLA YA KUIVAA MBAO FC JUNI 14 CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top