• HABARI MPYA

  Ijumaa, Juni 12, 2020

  SIMBA SC KUMKOSA MKUDE MECHI NA RUVU SHOOTING JUMAPILI BAADA YA KUUMIA DHIDI YA KMC

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC itamkosa kiungo wake tegemeo, Jonas Gerlad Mkude katika mchezo wake wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting Jumapili Uwanja wa Tafa Jijini Dar es Salaam. 
  Taarifa ya Simba SC leo imesema Mkude atakuwa nje ya Uwanja kwa muda wa wiki mbili baada ya kupata majeruhi kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya KMC wiki hii.
  Taarifa hiyo imesema kwamba kwa kipindi hiki kiungo huyo wa kimataifa wa Tanzania atakuwa akiendelea na mazoezi mepesi pamoja na matibabu.
  Ligi Kuu inatarajiwa kuanza tena kesho baada ya kusimama tangu Machi 17 kwa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutokana na mlipuko wa maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID 19.  
  Kesho Mwadui FC watakuwa wenyeji wa Yanga SC Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga wakati Coastal Union wataikaribisha Namungo FC Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
  Ligi itaendelea keshokutwa kwa Simba SC kuwakaribisha Ruvu Shooting Uwanja wa Taifa na Azam watakuwa wenyeji wa Mbao FC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Vigogo Yanga SC watahitmisha duru la mechi za viporo kwa kumenyana na JKT Tanzania Juni 17 Uwanja wa Taifa kabla Ligi Kuu kuanza tena rasmi Juni 20 na kufikia tamati Julai 26.  
  Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
  Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC KUMKOSA MKUDE MECHI NA RUVU SHOOTING JUMAPILI BAADA YA KUUMIA DHIDI YA KMC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top