• HABARI MPYA

  Jumanne, Juni 09, 2020

  KOCHA WA YANGA SC, MBELGIJI LUC EYMAEL SASA KUTUA NCHINI KESHO KUKIWEKA SAWA KIKOSI KABLA YA KUIVAA MWADUI JUMAMOSI

  Na Mwandshi Wetu, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mkuu wa Yanga SC, Mbelgiji Luc Eymael anatarajiwa kuwasili kesho saa 7:20 mchana tayari kuungana na kikosi kwa ajili ya kumalizia msimu.
  “Kocha Luc atawasili kwa ndege ya shirika la ndege la Lufthansa, akitokea nchini Ubelgiji ambako anaondoka leo mchana, atapitia Ujerumani, Ethiopia na kisha kutua Dar es Salaam,” amesema Hassan Bumbuli, Afisa Habari wa Yanga.
  Amesema mara baada ya kuwasili Uongozi unaandaa utaratibu ili kumuwezesha kocha kuungana na timu mjini Shinyanga na Dodoma.
  Kocha Luc amechelewa kurejea kutokana na hali ya usafiri wa anga nchini Ubelgiji na hivyo timu kuwa chini ya Kocha Msaidizi, Charles Boniface Mkwasa tangu ilipoanza mazoezi Mei 27.
  Baada ya kuchapwa 3-1 na KMC juzi katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, Yanga SC imerejea mazoezini Chuo cha Sheria, Oyster Bay kujiandaa na mechi za kumalizia msimu.
  Mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, watamenyana na Mwadui FC Jumamosi Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga katika mchezo wao wa kwanza wa kiporo, siku ambayo Coastal Union watakuwa wenyeji wa Namungo FC Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
  Yanga SC watashuka dimbani Juni 17 kumenyana na JKT Tanzania Uwanja wa Taifa.
  Mabingwa watetezi, Simba SC watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting Jumapili Uwanja wa Taifa, wakati Azam FC watakuwa wenyeji wa Mbao FC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
  Baada ya kukamilisha mechi hizo za viporo, rasmi Ligi Kuu itaanza Juni 20 na kufikia tamati Julai 26, mwaka huu baada ya kusimama tangu Machi 17, mwaka huu kwa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa maambukizi ya virusi vya corona duniani kote.  
  Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
  Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KOCHA WA YANGA SC, MBELGIJI LUC EYMAEL SASA KUTUA NCHINI KESHO KUKIWEKA SAWA KIKOSI KABLA YA KUIVAA MWADUI JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top