• HABARI MPYA

  Jumatatu, Juni 22, 2020

  AZAM FC YALALAMIKA KUNYIMWA MABAO MAWILI NA PENALTI DHIDI YA YANGA JANA TAIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  UONGOZI wa klabu ya Azam FC umesema kwamba haujaridhishwa na maamuzi ya waamuzi wa  mchezo wao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Yanga SC jana wakitoa suluhu Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
  Taarifa ya Azam FC kwenda Bodi ya Ligi iliyosainiwa na Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Abdulkarim Amin ‘Popat’ imemlaumu refa Heri Sasi na wasaidizi wake wawili, Soud Lila na Mbaraka Haule wote wa Dar es Salaam kwa kuwapendelea Yanga kimaamuzi.
  “Malalamiko haya yanatokana na nafasi tulizotengeneza kukataliwa kipindi cha kwanza dakika ya kwanza baada ya mpira wa krosi ya Idd Suleiman na goli kufungwa na Abdallah Kheri kukataliwa, nafasi ingine ilikuwa dakika ya 47 ya Idd Suleiman aliyetoa pasi kwa Never Tigere na goli kupatikana, lakini nafasi hizi mbili waamuzi walitafsiri ya kuwa wachezaji wetu walikuwa katika nafasi ya kuotea,” imesema taarifa hiyo.
  Aidha, taarifa hiyo imeongeza kwamba dakika ya 75 beki Mganda, Nico Wadada aliangushwa ndani ya eneo la penalti lakini cha kushangaza mwamuzi hakutoa penalti.
  “Haya matukio yamekuwa yakijirudia, tunaomba uchunguzi ufanyike na haki itendeke kwa mujibu wa sharia. Tunajua makosa mengine yanakuwa ni ya kibinadamu, ila tunaomba haki itendeke. Kuna vipande vya video vya mchezo huo kwa kujiridhisha tunavituma ili Kamati yako husika ivipitie na kutoa maamuzi,”imemalizia taarifa hiyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YALALAMIKA KUNYIMWA MABAO MAWILI NA PENALTI DHIDI YA YANGA JANA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top