• HABARI MPYA

  Jumatatu, Juni 22, 2020

  UONGOZI WA YANGA SC WASIKITISHWA NA MASHABIKI WANAOWAZOMEA WACHEZAJI NA KUPIGANA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Yanga imesikitishwa na vitendo vinavyoshamiri vinavyofanywa na baadhi ya mashabiki kwa kuzomea na kutukana baadhi ya wachezaji na hata kupigana wenyewe kwa wenyewe.
  “Kama uongozi tumesikitishwa sana na tunasisitiza umuhimu wa mashabiki kuiunga mkono timu yetu na wachezaji wetu lakini pia kupendana na kukosoana wao kwa wao kwa njia ya amani,”amesema Kaimu Katibu Mkuu, Wakil Simon Patrick.
  Amesema anafahamu kuna changamoto na mashabiki wanaumia, lakini kwa sasa ni muhimu zaidi kutoa ushirikiano wa hali na mali badala ya kuwachanganya wachezaji kisaikolojia na kugombana wenyewe kwa wenyewe jambo ambalo halina afya kwa ustawi wa Klabu na mpira kwa ujumla.
  "Sisi wana Yanga ndiyo tunatakiwa kuhakikisha tunawalinda wachezaji wetu dhidi ya mambo yote. Klabu ya Yanga imetajwa kuwa na mashabiki bora kinidhamu na kuheshimu wachezaji barani Afrika, hivyo ni muhimu sana kuendeleza Utamaduni wetu katika kuiunga mkono timu yetu,” amesema.
  Amesema Klabu inauhakikishia umma kuwa, itaendelea kuwalinda wachezaji wote kwa misingi ya usawa kama ilivyo dhima ya Klabu inayosisitiza upendo na amani michezoni.
  Aidha Klabu imewaomba Waandishi wa Habari hasa za mitandaoni kuzingatia kanuni na maadili ya kazi zao, kwani baadhi wameonekana kuwa chanzo cha kuvuruga utulivu wa timu kwa kuwahoji mashabiki ambao wamekuwa wakitoa lugha zisizofaa kwa wachezaji na uongozi. 
  Jana baada ya mchezo na Azam FC, baadhi ya mashabiki wa Yanga SC walikwenda kwenye basi kla timu na kumzomea na kumkashifu mshambulaji Muivory Coast, Gnamien Ghislain Yikpe aliyeingia dakika ya 64 kuchukua nafasi ya David Molinga.
  Yikpe alijiunga na Yanga SC Januari akitokea Gor Mahia ya Kenya, lakini kwa muda wote ameshindwa kuonyesha thamani yake Jangwani kiasi cha mashabiki kupoteza imani naye hadi kufikia kumzomea.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: UONGOZI WA YANGA SC WASIKITISHWA NA MASHABIKI WANAOWAZOMEA WACHEZAJI NA KUPIGANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top