• HABARI MPYA

    Saturday, June 20, 2020

    SIMBA SC YAFANYA KWELI TAIFA, YAICHAPA MWADUI FC 3-0 NA KUZIDI KUUSOGELEA UBINGWA LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imezidi kujisogeza karibu na taji la tatu mfululizo la Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Mwadui FC kwenye mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa Jijini Dar ed sSalaam.
    Kwa ushindi huo, Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Sven Ludwig Vandenbroeck inafikisha pointi 75 baada ya kucheza mechi 30, ikiendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi 15 zaidi ya Azam Fc inayofuatia nafasi ya pili. 
    Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Hance Mabena aliyesaidiwa na Mohamed Mkono na  Hamdani Said wote wa Tanga, hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0.

    Mabao hayo yalifungwa na kiungo Hassan Dilunga dakika ya tisa akimalizia pasi nzuri ya mshambuliaji na Nahodha, John Raphael Bocco na beki Augustino Simon aliyejifunga dakika ya 21 akijaribu kuokoa mpira uliopigwa na beki Shomari Kapombe kutoka upande wa kulia.
    Kipindi cha pili Mwadui FC walirudi na maarifa mapya na kufanikiwa kuwazuia Simba SC kupata mabao zaidi, lakini haikuwasaidia.
    Nahodha John Bocco akawainua wapenzi wa Simba SC dakika ya 58 akifunga bao la tatu akimalizia kwa kichwa mpira uliorudi baada ya kugonga mwamba kufuatia shuti la nyota kutoka Msumbiji, Luis Miquissone aliyepokea pasi ya Said Ndemla.  
    Mechi nyingine za Ligi Kuu leo; Ndanda SC imeshinda 1-0 dhidi ya Biashara United bao pekee la Abdul Hamisi dakika ya 90 na ushei kwa penalti Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
    JKT Tanzania imeshinda 2-0 dhidi ya Singida United, mabao ya Mussa Said dakika ya 11 na Hafidh Mussa dakika ya 61 Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma na Namungo FC imeichapa Kagera Sugar 2-0, mabao ya Hashim Manyanya dakika ya 14 na Reliants Lusajo dakika ya 77 Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.
    Bao pekee la Juma Nyangi dakika ya 19 limetosha kuipa ushindi wa ugenini wa 1-0 Alliance FC dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya, wakati KMC imeshinda 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Mabao ya KMC yamefungwa na Charles Ilamfya dakika ya 29 na Emmanuel Mvuyekure dakika ya 65, huku la Ruvu likifungwa na Graham Naftal dakika ya 53.
    Coastal Union imelazimishwa sare ya 0-0 Mtibwa Sugar Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga na Polisi Tanzania imelazimishwa sare ya 1-1 na Lipuli FC Uwanja wa Ushirika mjin Moshi mkoan Kilimanjaro. Polisi ilitangulia kwa bao la Baraka Majogoro dakika ya 50 kabla ya Rashid Hassan kuisawazishia Lipuli dakika ya 63.
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe/ Yusuph Mlipili dk73, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Kennedy Juma, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Gerson Fraga/Muzamil dk89 Yassin, Said Ndemla, John Bocco/ Meddie Kagere dk63, Luis Miquissone/ Clatous Chama dk63 na Hassan Dilunga/ Francis Kahata dk63.
    Mwadui FC; Mahmoud Amour, Mfaume Omar, Yahya Mbegu, Joram Mgeveke, Augustino Simon, Frank John/ Mussa Chambenga dk56, Ottu Joseph, Enrick Nkhosi, Raphael Aloba/ Maliki Jaffary dk68, Gerlad Mdamu na Herman Masenga/Omar Daga dk21.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAFANYA KWELI TAIFA, YAICHAPA MWADUI FC 3-0 NA KUZIDI KUUSOGELEA UBINGWA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top