• HABARI MPYA

  Jumatatu, Juni 01, 2020

  SIMBA KUANZA NA RUVU SHOOTING DAR, YANGA NA MWADUI FC SHINYANGA, AZAM NA MBAO CHAMAZI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BODI ya Ligi imetoa ratiba ya mechi za viporo za Ligi Kuu ya Tanzania na mabingwa watetezi, Simba SC watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting Juni 14 Uwanja wa Taifa, siku moja baada ya watani wao, Yanga kumenyana na Mwadui Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo amesema kwamba mechi za viporo zitaanza Juni 13 kwa Mwadui FC kuwakaribisha Yanga SC Shinyanga na Coastal Union kuwa wenyeji wa Namungo Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
  Juni 14, Azam FC watakuwa wenyeji wa Mbao FC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na Simba SC watawakaribisha Ruvu Shooting Dar es Salaam, wakati Juni 17, Yanga SC watakuwa wageni wa JKT Tanzania Uwanja wa Taifa.
  Kasongo amesema baada ya kukamilisha mechi hizo za viporo, rasmi Ligi Kuu itaanza Juni 20 na kufikia tamati Julai 26, mwaka huu.
  Ligi Kuu ilisimama Machi 17, mwaka huu TFF kwa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa corona duniani kote.  
  Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
  Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA KUANZA NA RUVU SHOOTING DAR, YANGA NA MWADUI FC SHINYANGA, AZAM NA MBAO CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top