• HABARI MPYA

  Jumanne, Juni 02, 2020

  MAKOCHA WAZUNGU AZAM FC KUANZA KUKINOA KIKOSI LEO CHAMAZI BAADA YA KUWASILI JANA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba jana amewasili nchini kutoka kwao, Romania na moja kwa moja kuanza kukinoa kikosi hicho kuelekea mchezo wao wa kiporo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Mbao FC Juni 14 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.
  Cioaba amerejea sambamba na Kocha wa Viungo, Costel Birsan, wakitokea mjini Frankfurt, Ujerumani walipounganisha usafiri wa ndege wa kuja Dar es Salaam.
  Wawili hao wataanza kesho leo jioni, kukinoa kikosi cha timu hiyo, ambacho tayari kilikuwa kimeanza mazoezi tangu Jumatano ya wiki iliyopita chini ya Kocha Msaidizi, Mrundi Bahati Vivier. 
  Makocha hao waliwasili siku ambayo Bodi ya Ligi imetoa ratiba ya mechi za viporo za Ligi Kuu baada ya mapumziko ya miezi miwili na ushei kufuatia mlipuko wa maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID 19.
  Ligi Kuu ilisimama Machi 17, mwaka huu TFF kwa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa corona duniani kote.  
  Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
  Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MAKOCHA WAZUNGU AZAM FC KUANZA KUKINOA KIKOSI LEO CHAMAZI BAADA YA KUWASILI JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top