• HABARI MPYA

  Jumatano, Juni 03, 2020

  YANGA SC WASHUGHULIKIA SUALA LA KOCHA WAO MBELGIJI, LUC EYMAEL KUREJEA NCHINI HARAKA

  Na Clement Shari, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Yanga ipo kwenye mchakato wa kuhakikisha kocha wake, Luc Eymael anarejea mapema nchini kutoka kwao, Ubelgiji alipokwenda kufunga ndoa ya tatu na kukwama kurejea mapema kutokana na mipaka yao kufungwa kwa sababu ya mlipuko wa maambukizi ya virusi vya corona.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa kampuni ya GSM, Mhandsi Hersi Said ambao wanaoisimamia klabu hiyo kuchelewa kurejea nchini kwa Luc kumetokana na kusimama kwa safari mbalimbali za ndege kufuatia janga la virusi vya corona.
  Aidha, Hersi amewatoa wasiwasi mashabiki wa Yanga SC ambao walikuwa na wasiwasi juu ya kukosekana kwa tiketi ya ndege ya kumrudisha Mwalimu huyo tayari kwa kuanza kuendelea na maandalizi ya kurejea kwa ligi kuu soka Tanzania Bara na mashindano mengine ya ubingwa.
  “Kocha wetu yupo nchini Ubelgiji kwa sasa, na alifunga safari ya kwenda Ubelgiji kwa tiketi ya kwenda na kurudi, tiketi hiyo ilimfanya kwenda na alivyofika kule akashughulika na mambo ya kifamilia ambayo alikuwa anahitaji kuyahudumia ikiwemo kufunga ndoa,”amesema Hersi na kuongeza;
  “Wote tunafahamu mipaka ya nchi zote ilifungwa na viwanja vingi vya ndege kufungwa, na wakati huo ndipo tiketi yake ikashindwa kufanya kazi kwa maana ya uwanja wa ndege ulikuwa umefungwa, sasa hivi viwanja vya ndege vimekwishafunguliwa na sasa hivi watu wa ndege wanashughulika na jinsi gani tiketi yake itapangiwa tarehe ya sasa,”.
  Ligi Kuu inatarajiwa kuanza tena Jun 13 baada ya kusimama tangu Machi 17, mwaka huu TFF kwa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa corona duniani kote.  
  Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
  Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC WASHUGHULIKIA SUALA LA KOCHA WAO MBELGIJI, LUC EYMAEL KUREJEA NCHINI HARAKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top