• HABARI MPYA

    Thursday, March 15, 2018

    LWANDAMINA ASEMA YANGA IPO VIZURI KUELEKEA MECHI NA TOWNSHIP ROLLERS JUMAMOSI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mzambia wa Yanga SC, George Lwandamina amesema kwamba kambi yake ipo vizuri kuelekea mchezo wa marudiano hatua ya 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Township Rollers keshokutwa mjini Gaborone.
    Yanga SC iliyofikia katika hoteli ya Crystal Palace mjini Gaborone inatarajiwa kuteremka Uwanja wa Taifa wa Gaborone Jumamosi Saa 9:45 na Saa 10:45 kwa saa za Afrika Mashariki kwa mchezo huo, wakihitaji ushindi wa 2-0 lazima ili kwenda hatua ya makundi baada ya kufungwa 2-1 Dar es Salaam Jumanne ya wiki iliyopita.
    Na akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo kwa simu kutoka Gaborone, Lwandamina amesema kwamba wanaendelea vizuri na maandalizi yao na wachezaji wote wapo vizuri.
    Kocha George Lwandamina (kulia) amesema timu yake ipo vizuri kuelekea mechi na Rollers Jumamosi

    “Tunamshukuru Mungu tunaendelea vizuri na maandalizi yetu, soka ya Afrika inafanana hata maeneo na vifaa vya mazoezi,”amesema.
    Kuhusu wagonjwa au majeruhi katika timu, Lwandamina amesema; “Soka ni mchezo wa nguvu hivyo huwezi kutarajia timu kutokuwa na mchezaji mwenye maumivu kabisa, kwa sababu Yanga imekuwa katika msimu mgumu huu,”.
    Wakati huo huo; Balozi wa Tanzania nchini Botswana, Sylvester Ambokile jana jioni hii aliitembelea kambi ya Yanga na kula chakula cha jioni na kuzungumza na wachezaji kuwapa moyo kuelekea mechi hiyo.
    Wachezaji waliopo na Yanga SC mjini Gaborone ni pamoja na makipa; Youthe Rostand, Ramadhani Kabwili, mabeki Juma Abdul, Gadiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Pato Ngonyani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani.
    Viungo ni Said Juma ‘Makapu’, Maka Edward, Yussuf Mhilu, Pius Buswita, Obrey Chirwa, Raphael Daudi, Juma Mahadhi, Ibrahim Ajib, Thabani Kamusoko, Emmanuel Martin na Geoffrey Mwashiuya.
    Upande wa viongozi ni pamoja na kocha Mkuu, Lwandamina, wasaidizi wake Mzambia mwenzake, Noel Mwandila na wazalendo Nsajigwa Shadrack, Juma Pondamali, Daktari Edward Bavu, Mchua Misuli Jacob Onyango na Meneja Hafidh Saleh wakati viongozi ni Omar Kaaya, Samuel Lukumay na Elias Mwanjala. 
    Balozi wa Tanzania nchini Botswana, Sylvester Ambokile akizungumza na wachezaji wa Yanga jana hotelini
    Balozi wa Tanzania nchini Botswana, Sylvester Ambokile alipiga picha ya ukumbusho pia na wachezaji wa Yanga 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LWANDAMINA ASEMA YANGA IPO VIZURI KUELEKEA MECHI NA TOWNSHIP ROLLERS JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top