• HABARI MPYA

  Jumatano, Machi 28, 2018

  MKUDE KURUDI MAZOEZINI KESHO SIMBA, MANARA ASEMA KIJANA HAJAUMIA SANA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIUNGO wa Simba SC, Jonas Mkude anaweza kuendelea na mazoezi kesho baada ya kuumia kifundo cha mguu juzi.
  Mkude alishindwa kuendelea na mazoezi juzi baada ya kugongana na kiungo mwenzake, Muzamil Yassin mazoezini Uwanja wa Boko Veterani, kiasi cha kubebwa hadi kwenye gari kabla ya kurudishwa nyumbani.
  Lakini baada ya vipimo jana, imegundulika mchezaji huyo aliyeibukia katika timu ya vijana ya Simba SC mwaka 2011 hajapata maumivu makubwa.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Haji Manara alisema Mkude hajaumia sana na atakuwa nje kwa muda wa siku mbili hadi tatu.
  Jonas Mkude (kulia) anaweza kuendelea na mazoezi kesho baada ya kuumia kifundo cha mguu juzi

  Alisema kwa taarifa alizopewa kutoka kwa daktari wa timu hiyo Yassin Gembe alisema kwamba kiungo huyo alipata mchubuko katika ngozi karibu ya mfupa wa enka.
  "Anaendelea vizuri na kutokana na jeraha sio kubwa amepewa siku mbili hadi tatu na kurejea kikosini kuendelea na mazoezi," alisema Manara.
  Simba inaendelea na mazoezi yake kwa kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Njombe Mji utakaochezwa katika Uwanja wa Sabasaba mjini humo Aprili 3.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MKUDE KURUDI MAZOEZINI KESHO SIMBA, MANARA ASEMA KIJANA HAJAUMIA SANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top