• HABARI MPYA

  Jumanne, Machi 27, 2018

  TAIFA STARS YAWAPA RAHA WANANCHI, YAWAPIGA KONGO 2-0…MAMBO YA SAMATTA NA KICHUYA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  TANZANIA imeonyesha inaweza baada ya kuifunga Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mabao 2-0 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Pongezi kwa wafungaji wa mabao hayo, Nahodha Mbwana Ally Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji na Shiza Ramadhani Kichuya wa Simba ya nyumbani yanayoipa ushindi wa kwanza Tanzania tangu Julai 7 mwaka jana ilipoichapa kwa matuta Lesotho baada ya sare ya 0-0 kwenye Kombe la COSAFA mjini Rusternburg, Afrika Kusini.
  Na wafungaji hao wote walisetiana, akianza Kichuya, mchezaji aliyeibuliwa Mtibwa Sugar ya Morogoro katika timu ya vijana, kabla ya kuivutia Simba SC mwaka juzi akiwa timu ya wakubwa na kusajiliwa kwa mamilioni na baadaye Samatta akajibu.
  Nahodha Mbwana Samatta akiwa amembeba Shiza Kichuya baada ya bao la pili leo 
  Mbwana Samatta akimiliki mpira mbele ya Aaron Tshibola wa DRC 
  Shiza Kichuya akijivuta kupiga shuti mbele ya Aaron Tshibola 
  Simon Msuva akipasua katikati ya mabeki wa DRC, Yannick Bangala (kushoto) na Wilfred Moke (kulia)  
  Ibrahim Ajib akiwatoka Yannick Bangala (katikati) na Wilfred Moke (kulia)  

  Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na marefa wa nyumbani, Elly Sasii aliyepuliza filimbi akisaidiwa na Ngazack Nduli na Mohamed Mkono, The Leopard ‘Chui wa DRC’ walikuwa wazuri kipindi cha kwanza na kukaribia mara kadhaa kufunga kama si ustadi wa safu ya ulinzi ya Stars chini ya mabeki Kelvin Yondan na Abdul Banda.
  Na baada ya dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza, Taifa Stars wakabadilika kipindi cha pili na kuanza kung’ara uwanjani.
  Alianza Nahodha na mshambuliaji wa zamani wa Simba ya nyumbani na TP Mazembe ya DRC, Samatta kuifungia Taifa Stars bao la kwanza dakika ya 74 kwa kichwa akimalizia krosi ya Kichuya kutoka upande wa kulia.
  Kichuya akaifungia Tanzania bao la pili dakika ya 88 akimalizia pasi ya Samatta baada ya kazi nzuri ya winga wa Difaa Hassan El Jadidi ya Morocco, Simon Msuva.
  Taifa Stars ilicheza vizuri kipindi cha pili hususan baada ya mabadiliko yaliyofanywa na kocha mzalendo, Salum Mayanga aliyewaingiza Ibrahim Ajib na Mudathir Yahya kuchukua nafasi za Mohammed Issa ‘Banka’ na Himid Mao.
  Tanzania iliingia kwenye mchezo wa leo ikitoka kufungwa 4-1 na Algeria mjini Algiers Machi 22 katika mchezo mwingine wa kirafiki na kwa ujumla huu ni ushindi wa kwanza kwa Taifa Stars ndani ya mechi 10, ikifungwa nne na sare tano.   
  Taifa Stars ilitoa sare mbili mfululizo na Rwanda kufuzu Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), 1-1 Julai 15 mjini Mwanza na 0-0 Julai 22 mjini Kigali, kabla ya kutoa sare nyingine za 1-1 mfululizo na Malawi mjini Dar es salaam Oktoba 7 na Benin Novemba 12.
  Ikatoa sare ya 0-0 na Libya Desemba 3, ikafungwa 2-1 mara mbili, kwanza na Zanzibar Desemba 7, baadaye na Rwanda Desemba 9 na 1-0 na Kenya Desemba 11 kwenye michuano ya Challenge mjini Nairobi.
  Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Tanzania: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gardiel Michael, Abdi Banda, Kelvin Yondan, Himid Mao/Mudathir Yahya dk73, Mohammed Issa ‘Banka’/Ibrahim Ajib dk59, Erasto Nyoni, Mbwana Samatta, Simon Msuva/Yahya Zayed dk90 na Shiza Kichuya/Rashid Mandawa dk87. 
  DRC; Ley Matampi, Issam Mpeko, Glody Ngoda, Yannick Bangala, Wilfred Moke, Aaron Tshibola/Lema Mabibi dk46, Chancel Mbemba, Mubele Ndombe/Junior Kabananga dk54, Needkens Kebano, Bennick Afobe/Assombalanga Britt dk63 na Yannick Bolasie.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TAIFA STARS YAWAPA RAHA WANANCHI, YAWAPIGA KONGO 2-0…MAMBO YA SAMATTA NA KICHUYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top