• HABARI MPYA

  Jumatatu, Machi 19, 2018

  KOCHA MFARANSA WA SIMBA SIMBA SC AONDOKEA CAIRO KUREJEA KWAO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imerejea leo Dar es Salaam kutoka Misri, ambako Jumamosi kilitolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua 32 Bora baada ya sare ya 0-0 katika mchezo wa marudiano na wenyeji, Al Masry Uwanja wa Port Said.
  Lakini kocha wake Mkuu, Mfaransa Pierre Lechantre ameondokea Cairo kwenda kwao, Ufaransa kwa kile kilichoelezwa mapumziko mafupi.
  Kikosi kizima na makocha wote Wasaidizi, Mtunisia Mohammed Aymen Hbibi, Mrundi Masoud Juma na mzalendo, Muharami Mohammed ‘Shilton’ kimerejea Dar es Salaam na wachezaji wamepewa mapumziko mafupi hadi Jumamosi.
  Pierre Lechantre (kushoto) ameondokea Cairo kurejea kwao, Ufaransa kwa mapumziko mafupi

  Wachezaji wanne, kipa Aishi Manula, mabeki Shomari Kapombe na Erasto Nyoni na viungo Said Ndemla na Shiza Kichuya nao pia walioondokea Cairo kwenda Algeria kuungana na timu ya taifa, Taifa Stars ambayo Alhamisi itacheza mchezo wa kirafiki na wenyeji, The Greens.
  Sare ya 0-0 Jumamosi inaifanya Simba SC itolewe kwa mabao ya ugenini kwenye Kombe la Shirikisho kufuatia sare ya 2-2 katika mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam Machi 7.
  Hii inakuwa michuano ya pili Simba kutolewa msimu huu, baada ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) na sasa Simba SC wanaelekeza nguvu zao kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambako wanaongoza.
  Simba SC ina pointi 46 baada ya kucheza mechi 20, wakati mabingwa watetezi, Yanga SC wanafuatia kwa pointi zao 46 pia baada ya kucheza mechi 21, lakini wanazidiwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
  Kwa sasa Ligi Kuu imesimama kwa muda mechi za kimatafa zilizo katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na mechi za Robo Fainali ya Azam Sports Federation (ASFC).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KOCHA MFARANSA WA SIMBA SIMBA SC AONDOKEA CAIRO KUREJEA KWAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top