• HABARI MPYA

  Alhamisi, Machi 29, 2018

  SIMBA SC WAENDA KUWEKA KAMBI IRINGA MECHI NA NJOMBE MJI FC JUMANNE SABA SABA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC inatarajiwa kuondoka Jumamosi kwenda kuweka kambi Iringa kwa siku mbili kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Njombe Mji FC Jumanne.
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Hajji Sunday Manara amesema kwamba Simba itakuwa Iringa Jumamosi hadi mapema Jumatatu itakaposafiri kwenda Njombe.
  “Timu itasafiri kwenda Njombe Jumamosi hii kupitia Iringa ambako itaweka kambi hadi Jumatatu, kabla ya mechi ya Jumanne ya tarehe tatu Aprili. “Tunaamini tutashinda inshaallah, muhimu dua na sala zenu. Mtupokee nyanda za juu kusini mwa Tanzania,”amesema Manara.
  Katika mchezo huo, Simba SC itamkosa kiungo wake tegemeo wa ulinzi, Jonas Mkude ambaye aliumia kifundo cha mguu wiki hii mazoezini Uwanja wa Boko Veterani, Dar es Salaam.
  Itaendelea pia kumkosa Nahodha wake, mshambuliaji John Raphael Bocco ‘Adebayor’ ambaye ni majeruhi sawa na beki, Salim Mbonde na kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.
  Simba SC watakuwa wageni wa Njombe Mji FC Aprili 3, mwaka huu Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe katika mfululizo wa Ligi Kuu wakitoka kutolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na AL Masry ya Misri.
  Simba ilitoa sare ya 0-0 na Al Masry Machi 17 na kutolewa kwa mabao ya ugenini baada ya sare ya 2-2 Machi 7, mwaka huu kwenye mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika.
  Na baada ya kutolewa kwenye michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) Novemba mwaka jana wakifungwa na Green Warriors ya Mwenge kwa penalti baada ya sare ya 1-1, Simba SC wana nafasi moja tu kucheza michuano ya Afrika mwakani, ambayo ni kupitia Ligi Kuu ambako bingwa wake hucheza Ligi ya Mabingwa Afrika. 
  Na bahati nzuri kwao, Simba SC ndiyo wanaoongoza Ligi Kuu kwa wastani wao mzuri wa mabao baada ya kulingana kwa pointi na mabingwa watetezi, Yanga SC 46 kila timu, ingawa pia Wekundu wa Msimbazi wana mechi moja mkononi.   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC WAENDA KUWEKA KAMBI IRINGA MECHI NA NJOMBE MJI FC JUMANNE SABA SABA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top