• HABARI MPYA

  Jumanne, Machi 27, 2018

  TFF KIBOKO, JANA IMETOA RATIBA MPYA YA LIGI KUU, LEO ‘IMEFUMULIWA’ TENA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KATIKA hali ya kustaajabisha mno, Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imefanya marekebisho madogo katika ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara siku moja tu baada ya kutoa ratiba iliyorekebishwa.
  Kwa mara ya sita, au zaidi jana Bodi ilitoa ratiba mpya kuanzia mzunguko wa 23, ikijumuisha pia mechi tatu za viporo vya Yanga dhidi ya Mtibwa Sugar na Simba SC dhidi ya Njombe Mji FC na Mtibwa Sugar.
  Lakini ajabu leo tena Bodi imetuma taarifa ya marekebisho ya mchezo mmoja tu wa Ligi Kuu, mechi namba 199 kati ya Mbeya City na Yanga iliyopangwa kufanyika Mei 1, 2018 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya ambayo sasa itapangiwa tarehe nyingine.
  Taarifa ya Bodi imesema kwamba uamuzi wa kuipangia tarehe nyingine ni kukidhi matakwa ya Kanuni inayotaka nafasi kati ya mechi moja na nyingine isiwe chini ya angalau saa 72.
  Kwa mujibu wa ratiba, Yanga itakuwa na mechi dhidi ya Simba itakayofanyika Aprili 29, 2018 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
  Mechi nyingine zilizopangiwa tarehe ni za viporo zinazowahusu vigogo, Simba na Yanga hao ambazo ziliahirishwa wiki iliyopita kupisha mechi za marudiano za Raundi ya Kwanza michuano ya Afrika.
  Hizo ni kati ya Njombe Mji FC na Simba SC uliokuwa ufanyike Machi 11 Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe ambao sasa utachezwa Aprili 3 na Mtibwa Sugar dhidi ya Yanga SC, uliokuwa ufanyike Machi 3, sasa utachezwa Mei 9 Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TFF KIBOKO, JANA IMETOA RATIBA MPYA YA LIGI KUU, LEO ‘IMEFUMULIWA’ TENA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top