• HABARI MPYA

    Sunday, March 25, 2018

    WELAYTA DICHA ITATOLEWA KWA MAANDALIZI MAZURI NA SI KWA SABABU NI TIMU YA ETHIOPIA

    YANGA wana imani kubwa watafuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika mwaka huu, baada ya kupangwa na timu ya Welayta Dicha ya Ethiopia katika mechi mbili za nyumbani na ugenini za mchujo wa kuwania kuingia hatua hiyo.
    Katika droo iliyokwenda sambamba na upangwaji wa makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika Jumatano wiki hii mjini Cairo, Misri, Yanga wataanzia nyumbani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Aprili 7 kabla ya kwenda Addis Ababa kwa mchezo wa marudiano Aprili 17 au 18, mwaka huu.
    Welayta Dicha watakuwa wanakuja Tanzania kwa mara ya pili mwaka huu, baada ya Februari kuja kucheza na na Zimamoto ya Zanzibar na kushinda kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoa sare ya 1-1 Uwanja wa Amaan, kabla ya kushinda 1-0 Erthiopia.
    Yanga SC imeangukia kwenye mchujo huo baada ya kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 2-1 iliyofungwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya sare 0-0 kwenye mchezo wa marudiano na wenyeji, Township Rollers Uwanja wa Taifa mjini Gaborone nchini Botswana.
    Welayta Dicha imefika hatua hii baada ya kuitoa Zamalek ya Misri kwa penalti 4-3 baada ya sare ya jumla ya 3-3, kila timu ikishinda 2-1 nyumbani kwake.
    Katika Raundi ya Awali ambayo Yanga SC iliitoa Saint Louis Suns United ya Shelisheli kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Dar es Salaam na sare ya 1-1 Mahe, Welayta Dicha iliitoa Zimamoto ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoa sare ya 1-1 Uwanja wa Amaan, kabla ya kushinda 1-0 Erthiopia.
    Huu ni mwaka wa tatu mfululizo, Yanga inaangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na mara ya nne kwa ujumla kihiostoria.
    Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2007 ilipotolewa na na El Merreikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-0 iliyofungwa Khartoum baada ya sare ya 0-0 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
    Iliingia kwenye kapu hilo baada ya kutolewa na  Esperance ya Tunisia katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mabao 3-0 iliyofungwa mjini Tunis, baada ya sare 0-0 Mwanza.
    Mwaka pekee Yanga ilifuzu hatua ya makundi Kombe la Shrikisho Afrika baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa ni 2016, ilipoitoa Sagrada Esperança ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1, ikishinda 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa 1-0 Angola.
    Hiyo ilikuwa baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kwenda kufungwa 2-1 Alexandria.
    Katika hatua ya makundi, Yanga ilipangwa Kundi moja na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), MO Bejaia ya Algeria na Medeama SC ya Ghana. 
    Yanga ilishinda mechi moja tu dhidi ya MO Bejaia 1-0 na sare ya 1-1 na Medeama Dar es Salaam huku mechi nyingine zote nne ikifungwa, zikiwemo mbili za nyumbani na ugenini na TP Mazembe.
    Mwaka jana pia Yanga baada ya kutolewa na Zanaco ya Zambia kwa mabao ya ugenini, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na 0-0 Lusaka, ikaenda kutolewa na MC Alger ya Algeria kwa jumla ya mabao 4-1 kwenye mchujo wa kuwania tiketi ya hatua ya makundi Kombe la Shirikisho, ikishinda 1-0 Dar es Sakaam na kufungwa 4-0 Algiers.
    Tangu Welayta Dicha kujitokeza kama mpinzani wa Yanga katika hatua hii, imani ya viongozi wa timu hiyo imekuwa kubwa kwamba hiyo ni njia ya mkato kwao kwenda hatua ya makundi.
    Yanga wanaamini Welayta Dicha, timu kutoka Ethiopia haiwezi kuwa kikwazo kwao kwa sababu wanaichukulia kama timu ya kawaida, japo hawajui ubora wao uliowawezesha kuitoa Zamalek.
    Kweli Yanga ina rekodi nzuri za kukumbukwa dhidi ya timu za Ethiopia, ikiwemo ile ya mwaka 1998 walipoitoa Coffee kwa jumla ya mabao 8-3, wakianza na sare ya 2-2 ugenini kabla ya kuja kushinda 6-1 Dar es Salaam, hivyo kukata tiketi ya kwenda hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ta kwanza katika historia yao.
    Na waliitoa Coffee ikitoka kuitoa timu nyingine kigogo cha Misri, Al Ahly kwa mabao ya ugenini baada ya sare ya 1-1 Ethiopia na 2-2 Cairo.
    Hii inawapa jeuri Yanga waamini wataitoa tu Welayta Dicha kwa sababu ni timu ya Ethiopia bila kuzingatia ubora wake. Wakati mwingine timu zetu hutolewa na timu dhaifu mashindanoni tu kwa hofu yao kwa sababu zinatoka labda Kaskazini au Magharibi mwa Afrika na pia hutolewa mashindanoni na timu nyingine kwa sababu tu ya kuzidharau kutokana na nchi zinazotoka.
    Wengi wanaamini Yanga imetolewa na Township Rollers kwa uzembe tu na kielelezo ni kiwango cha timu na matokeo ya 0-0 katika mchezo wa marudiano baada ya kufungwa 2-1 kwenye mchezo wa kwanza Dar es Salaam, ambao timu haikuwa na maandalizi mazuri wakiamini wana mechi nyepesi.
    Wakati umefika viongozi wa klabu zetu waondokane na desturi ya kuendesha mambo kwa dhana badala ya hali halisi, kwa sababu timu za Ethiopia ambazo Yanga wanazidharau zimewahi kuiadhiri timu hiyo hapa hapa Dar es Salaam.  
    Ni mwaka 2011 tu katika Raundi ya Awali Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga iliponea chupuchupu kupata kipigo kikali kutoka kwa Dedebit ya Ethiopia Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, ikitoka nyuma kwa mabao 4-0 hadi mapumziko na kupata sare ya 4-4 baada ya kusawazisha kipindi cha pili.
    Na hiyo ndiyo ilikuwa timu ya mwisho ya Ethiopia kucheza na Yanga kwenye michuano ya Afrika – lakini leo wakipangwa tena na timu kutoka nchi hiyo wanajipa matumaini wamepata njia ya mkato ya kwenda hatua ya makundi.
    Hata mimi naamini Welayta Dicha ipo ndani ya uwezo wa Yanga, lakini si kwa maneno kama inavyoendelea sasa na kusubiri miujiza, au bahati ifanye kazi.
    Yanga wanatakiwa kufanya kazi ya kuiandaa timu yao na kujiandaa kumenyana na Welayta Dicha, kwa kuhakikisha wanacheza na timu wanayoijua na si kwenda kubahatisha matokeo uwanjani.
    Yanga wanapaswa kupata CD za Welayta Dicha katika mechi zao za hivi karibuni, hususan dhidi ya Zamalek ili kuifahamu timu hiyo inachezaje, ina wachezaji wa aina gani na ni akina nani hatari zaidi. Hiyo ndiyo mipango ya soka. 
    Motisha kwa wachezaji wa Yanga wenyewe kabla ya mchezo huo ni muhimu, kuliko kutoa ahadi eti wakishinda watapewa nini. Lazima wachezaji wafurahie kambi ya maandalizi kuelekea mechi hiyo na viongozi wawe karibu na timu, hususan Kaimu Mwenyekiti, Clement Sanga.
    Sanga asiwaachie timu akina Hussein Nyika na Samuel Lukumay peke yao, naye awe karibu na timu katika maandalizi asikilize shida na maoni ya wachezaji. Yanga wajue kwamba mpira hauchezwi mdomoni tena. Bin Zubeiry naamini Welayta Dicha itatolewa kwa maandalizi mazuri na si kwa sababu ni timu ya Ethiopia.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WELAYTA DICHA ITATOLEWA KWA MAANDALIZI MAZURI NA SI KWA SABABU NI TIMU YA ETHIOPIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top