• HABARI MPYA

  Jumatatu, Machi 26, 2018

  TFF YAPANGUA TENA RATIBA YA LIGI KUU, SIMBA NA YANGA SASA APRILI 29

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) kupitia Bodi ya Ligi, limetoa ratiba mpya ya marekebisho ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ikionyesha mchezo baina ya mahasimu wa jadi, Simba na Yanga sasa utachezwa Aprili 29, mwaka huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Mechi nyingine zilizopangiwa tarehe ni za viporo zinazowahusu vigogo hao ambazo ziliahirishwa wiki iliyopita kupisha mechi za marudiano za Raundi ya Kwanza michuano ya Afrika.
  Hizo ni kati ya Njombe Mji FC na Simba SC uliokuwa ufanyike Machi 11 Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe ambao sasa utachezwa Aprili 3 na Mtibwa Sugar dhidi ya Yanga SC, uliokuwa ufanyike Machi 3, sasa utachezwa Mei 9 Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
  Mechi nyingine ni kati ya Mtibwa Sugar na Simba SC ambayo sasa itachezwa Aprili 9, mwaka huu Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. 
  Taarifa ya Bodi ya Ligi inakuja siku mbili baada ya uongozi wa Njombe Mji FC kusema haujapokea taarifa yeyote kuhusu mabadiliko ya mchezo wao.
  Msemaji wa Njombe Mji FC, Hassan Mancho, amesema kwamba taarifa zinazosambazwa mitandaoni na kwenye baadhi ya vyombo vya habari, mpaka sasa hazina uthibitisho wowote.
  “Kanuni ya Ligi Kuu inatamka kwamba taarifa za mabadiliko ya mchezo zitatolewa kwa klabu siku 14 kabla ya mchezo husika. Timu ya Njombe mji haijapokea taarifa kuhusu mchezo huo kuchezwa Aprili 3, 2018,”amesema.
  “Hii itakuwa njia ya kutuondoa kwenye ligi, haiwezekani tukacheze Shinyanga, siku mbili halafu turudi Njombe kisha turudi tena Shinyanga siku mbili baadaye. Kanuni inataka tupate taarifa siku kumi na nne kabla, leo hata tukipewa kesho basi siku hizo hazikidhi kwa mujibu wa kanuni" amesema Macho.
  Kwa sasa inajiandaa na safari ya Shinyanga kwa michezo miwili dhidi ya Stand United, wa Robo Fainali ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) Machi 30 na wa Ligi Kuu Aprili 8, zote zikipigwa Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
  Baada ya hapo, Njombe wanasema ratiba itawapeleka Mwanza kwa mchezo na Mbao Aprili 11, kabla ya kwenda Dar es Salaam kumenyana na Azam FC Aprili 15 kisha kurejea nyumbani mjini Mjombe kucheza na Ndanda FC.
  Awali Bodi ya Ligi ya TFF iliusogeza mbele mchezo kati ya Njombe Mji FC na Simba SC uliopangwa kufanyika Machi 11 Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe.
  Hiyo ilifuatia Simba kuomba mchezo huo uahirishwe ili wapate fursa nzuri ya maandalizi kwa ajili ya mchezo wake wa marudiano Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry mjini Port Said Machi 17.
  Simba ililazimisha sare ya 0-0 na Al Masry Machi 17 mjini Port Said na kutolewa kwa mabao ya ugenini baada ya sare ya 2-2 kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na sasa inarejesha nguvu zake kwenye Ligi Kuu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TFF YAPANGUA TENA RATIBA YA LIGI KUU, SIMBA NA YANGA SASA APRILI 29 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top