• HABARI MPYA

  Jumatano, Machi 21, 2018

  AZAM FC KUCHEZA NA FRIENDS RANGERS JUMAMOSI, BEKI MGHANA KUTIBIWA AFRIKA KUSINI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Azam FC inatarajiwa kunoa makali yake kwa kukipiga na Friends Rangers ya kwenye mchezo wa kirafiki Jumamosi Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kuanzia Saa 1:00 usiku.
  Mchezo huo ni maalum kabisa kwa ajili ya kuwaweka wachezaji kwenye ushindani kutokana na kusimama kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kupisha mechi za Kimataifa za kirafiki zilizo katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
  Aidha Azam FC inayoendelea na mazoezi makali kwenye viunga vyake vya Azam Complex, itautumia mchezo huo kama sehemu ya kujiweka sawa kuelekea mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Mtibwa Sugar utakaofanyika uwanjani hapo Machi 31 mwaka huu saa 1.00 usiku.

  Daniel Amoah aliumia Desemba 19, mwaka jana katika mechi ya kirafiki dhidi ya Polisi Tanzania, Azam FC ikishinda  3-1

  Wakati huo huo, beki wa kati wa Azam FC, Mghana Daniel Amoah, anatarajiwa kwenda mjini Cape Town, Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu ya goti Jumatatu ijayo.
  Amoah ameshindwa kupona majeraha hayo tokea ayapate Desemba 19, mwaka jana, wakati Azam FC ikicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Polisi Tanzania na kuichapa mabao 3-1.
  Februari 7 alirejea tena uwanjani na kucheza mechi dhidi ya Simba, Azam FC ikipoteza kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, ambapo alijikuta akijitonesha tena hali iliyomfanya kukaa nje ya dimba hadi sasa.
  Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa, amesema kwamba beki huyo ataenda kutibiwa katika Hospitali ya Vincent Pallotti iliyopo nchini humo na akiangaliwa kwa undani tatizo lake kwa muda wa siku nne.
  “Daniel Amoah analalamika au ana tatizo la maumivu makali katikati ya goti kwa hiyo timu ya Azam inampeleka Afrika Kusini kwa matibabu na uchunguzi zaidi na atakwenda Cape Town Jumatatu ijayo katika Hospitali ya Vincent Pallotti kuonana na Daktari bingwa wa mifupa Dr. Nickolas na atakaa huko kwa muda wa siku nne na itategemeana kama tatizo litakuwa ni kubwa basi ataongezewa muda wa kukaa huko,” alisema.
  Beki huyo wa zamani wa Medeama ya Ghana aliyesajiliwa na Azam FC msimu uliopita, anakuwa mchezaji wa nne wa timu hiyo msimu huu kupelekwa Afrika Kusini kwa matibabu, awali mwaka jana walipelekwa Josepha Kimwaga, Shaaban Idd kufanyiwa upasuaji kabla ya wiki nne zilizopita nahodha Himid Mao ‘Ninja’ naye kupelekwa kwa uchunguzi wa goti lake na sasa akiwa fiti kabisa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC KUCHEZA NA FRIENDS RANGERS JUMAMOSI, BEKI MGHANA KUTIBIWA AFRIKA KUSINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top